Latest Posts

MADAKTARI KENYA WAPANGA MGOMO TENA, WADAI SERIKALI IMESHINDWA KUTIMIZA AHADI

Muungano wa madaktari nchini Kenya umetangaza rasmi ilani ya mgomo wa siku 21, wakitaka serikali kutekeleza makubaliano ya utendakazi waliyofikia mwaka 2017. Mgomo huo unatarajiwa kuanza tarehe 22 Desemba iwapo serikali haitachukua hatua za kushughulikia changamoto zinazowakumba madaktari nchini humo.

Kulingana na Shirika la habari la BBC, tangazo hili linakuja miezi michache baada ya mgomo wa awali uliowahusisha madaktari takriban 4,000 kutoka hospitali za umma mnamo Machi 14 mwaka huu. Mgomo huo ulilenga kushinikiza ajira kwa madaktari wapya, kuboresha mazingira ya kazi, na kuhakikisha upatikanaji wa mafunzo bora ya kitaaluma.

Mgomo wa Machi ulisitishwa baada ya siku 56, kufuatia mazungumzo yaliyowaleta madaktari na serikali kwenye makubaliano tarehe 8 Mei. Hata hivyo, hadi sasa, serikali haijatekeleza sehemu kubwa ya ahadi ilizotoa, hali ambayo imewaacha madaktari katika hali ya kukata tamaa.

“Tulirejea kazini kwa imani kwamba serikali itatekeleza ahadi zake, lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa,” amesema mmoja wa wawakilishi wa muungano wa madaktari.

Madaktari matarajali, ambao hufanya kazi kwa mwaka mmoja kabla ya kupata leseni ya kudumu, wameeleza hali ya dhiki wanayokabiliana nayo kazini. Wanalalamikia saa nyingi za kazi, mazingira magumu, na kutolipwa mishahara yao kwa muda mrefu.

Muungano wa madaktari umetoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka ili kuepusha mgomo wa Desemba. Wanasisitiza kuwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya awali ni ishara ya kupuuza maslahi ya sekta ya afya, jambo linalohatarisha huduma za afya kwa mamilioni ya Wakenya.

“Serikali inapaswa kuonesha uongozi wa kweli kwa kutimiza makubaliano haya kabla ya mgomo kuanza,” ameongeza msemaji wa muungano huo.

Kwa upande wa serikali, bado hakuna tamko rasmi kuhusu tangazo hilo la mgomo. Hali hii inazua wasiwasi juu ya mustakabali wa huduma za afya katika kipindi cha msimu wa sikukuu.

Mgomo wa mara kwa mara wa madaktari nchini Kenya umeibua mjadala mkubwa kuhusu uwekezaji wa serikali katika sekta ya afya. Pamoja na kuahidi kuboresha sekta hiyo, serikali inakosolewa kwa kushindwa kushughulikia changamoto za msingi zinazowakumba wahudumu wa afya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!