Latest Posts

MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA UHALIFU YASEMA MONGOLIA WANA WAJIBU WA KUMKAMATA PUTIN

Maafisa wa Mongolia wamesisitizwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuwa na “wajibu” wa kumkamata Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ikiwa atazuru nchi hiyo wiki ijayo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC Swahili, Safari hiyo, inayotarajiwa kufanyika Jumanne itakuwa ni mara ya kwanza kwa Putin kutembelea nchi mwanachama wa ICC tangu mahakama hiyo kutoa kibali cha kumkamata mwezi Machi 2023.

Mahakama hiyo inamtuhumu Putin kwa uhalifu wa kivita, ikidai kuwa alishindwa kuzuia ufurushwaji haramu wa watoto kutoka Ukraine hadi Urusi tangu kuzuka kwa mzozo kati ya nchi hizo mbili. Maafisa nchini Ukraine wamekuwa wakitoa wito kwa Mongolia kumkamata Putin mara tu atakapowasili nchini humo.

Hata hivyo, Kremlin imejibu kuwa haina wasiwasi kuhusu ziara hiyo. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alieleza kuwa Urusi ina uhusiano mzuri na Mongolia, akisema, “Bila shaka, vipengele vyote vya ziara ya Rais vimetayarishwa kwa makini.”

Naye Msemaji wa ICC, Dkt Fadi el-Abdallah alieleza kuwa mahakama hiyo inategemea ushirikiano kutoka kwa nchi wanachama wake, ikiwa ni pamoja na Mongolia, ili kutekeleza maamuzi yake. Aliongeza kuwa Mongolia ina wajibu wa kushirikiana na mahakama hiyo, ikiwa ni pamoja na kufuata kibali cha kumkamata Putin.

Mbali na Putin, ICC pia imetoa kibali cha kukamatwa kwa Maria Lvova-Belova, kamishna wa haki za watoto wa Urusi kwa mashtaka yanayofanana na yale yanayomkabili Putin. Uhalifu huu unadaiwa kufanyika Ukraine tangu tarehe 24 Februari 2022, wakati Urusi ilipoanzisha uvamizi wake.

Moscow imekanusha madai hayo na kuyataja kuwa “ya kuudhi.” Dkt Abdallah alibainisha kuwa ICC itaendelea kufuatilia nchi wanachama wake ambao hawatashirikiana, na majaji wa mahakama hiyo wataarifu Bunge la Nchi Wanachama, ambalo linaweza kuchukua hatua stahiki.

Mahakama ya ICC haina mamlaka ya moja kwa moja ya kuwakamata washukiwa na inategemea ushirikiano wa nchi wanachama wake ili kutekeleza maamuzi yake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!