Latest Posts

MAHAKAMA YA ULAYA: KUKATAA KUFANYA MAPENZI SIYO SABABU YA TALAKA

Mahakama Kuu ya Haki za Binadamu ya Ulaya (ECHR) imeamua kwamba kukataa kufanya mapenzi hakupaswi kuwa msingi wa talaka, katika rufaa iliyoshinda mwanamke mmoja wa Ufaransa aliyejulikana kama H.W.

Mahakama hiyo imesema Ufaransa ilikiuka haki ya H.W. ya kuishi kwa heshima, kama ilivyoainishwa katika sheria za haki za binadamu. H.W., ambaye alikumbana na changamoto nyingi za ndoa na matatizo ya kiafya, amesema uamuzi huo unathibitisha haja ya kuhamasisha makubaliano na usawa wa kijinsia katika ndoa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC, H.W., mwenyeji wa Le Chesnay karibu na Paris, aliolewa mwaka 1984 na JC, ambapo walibarikiwa na watoto wanne, mmoja wao akiwa na ulemavu unaohitaji huduma ya mara kwa mara. Baada ya miaka mingi ya ndoa, mahusiano yao yalidorora, na H.W. alianza kukumbana na ukatili wa kimwili na wa kisaikolojia kutoka kwa mumewe. Mwaka 2004, alikataa kuendelea na mahusiano ya kimapenzi naye, hali iliyosababisha talaka mwaka 2012.

Hata hivyo, msingi wa talaka hiyo ulikuwa kwamba H.W. alikataa kutimiza kile kilichoitwa “wajibu wa ndoa.” Mwanamke huyo hakupinga talaka lakini alikosoa msingi huo kisheria, akisema kuwa ni wa zamani na hauna nafasi katika jamii ya kisasa.

Kesi hii imeibua mjadala mkubwa nchini Ufaransa kuhusu makubaliano ya ndoa na haki za wanawake. Wakili wa H.W., Lilia Mhissen, amesema uamuzi huo unavunja dhana ya zamani ya “wajibu wa ndoa” na unatoa nafasi kwa mtazamo wa kisasa zaidi unaoendana na heshima ya binadamu.

Ripoti ya hivi karibuni ya wabunge wa Ufaransa pia imependekeza kuingiza dhana ya kukataa makubaliano katika tafsiri ya ubakaji wa kisheria, ikisisitiza kuwa makubaliano lazima yawe ya hiari na yanaweza kubatilishwa wakati wowote.

Vikundi vya kutetea haki za wanawake vimekaribisha uamuzi huu kama hatua muhimu ya kumaliza kile walichokiita “utamaduni wa ubakaji” na kuhimiza mazungumzo zaidi juu ya haki, usawa, na makubaliano ndani ya ndoa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!