Kundi la kisiasa linaloungwa mkono na Elon Musk linaweza kuendelea kutoa zawadi ya dola milioni moja kwa wapiga kura katika majimbo muhimu yatakayokuwa na nafasi ya kuamua mshindi wa uchaguzi wa urais wa Marekani, kufuatia uamuzi wa jaji wa Pennsylvania.
Zawadi hiyo, ambayo inatekelezwa na kundi la Bw. Musk lijulikanalo kama America PAC, ilikuwa imepangwa kumalizika Jumanne, huku mpokeaji wa mwisho wa kiasi hicho akiwa tayari amewekwa bayana, kulingana na wakili wa Musk.
Katika taarifa ya kushangaza iliyotolewa mahakamani, wakili huyo alifichua kuwa wapokeaji wa fedha hizo walichaguliwa moja kwa moja na kundi hilo, na sio kupitia njia ya bahati nasibu kama ilivyokuwa ikidhaniwa na wengi.
Wakili wa Wilaya ya Philadelphia, Lawrence Krasner, alikuwa amefungua kesi ya kupinga zawadi hizo, akiziita “bahati nasibu isiyo halali,” baada ya Musk kutangaza kuwa zawadi hiyo ya mamilioni ya dola ingewafikia wapiga kura kila siku hadi kufikia siku ya Uchaguzi.
Jaji Angelo Foglietta hakutoa sababu mara moja ya uamuzi wake, lakini aliruhusu kundi hilo kuendelea kutoa zawadi hizo. Wakili wa Musk, Chris Gober, alithibitisha kuwa mpokeaji wa mwisho wa dola milioni moja tayari amechaguliwa, na kwamba atatoka katika jimbo la Michigan. Siku ya Jumatatu, kundi hilo lilitangaza mshindi wa siku hiyo, Joshua kutoka Arizona, kama mpokeaji wa zawadi.