Waziri Mkuu wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kassim Majaliwa amewataka Wanaliwale kuwachagua wagombea wote wa CCM kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa Chama hicho kimechagua majembe.
Amesema kuwa kama ilivyo kwa uimara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi wa mwenyekiti wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kilichagua wagombea wazuri wenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ili kuwaletea Watanzania maendeleo.
Amesema hayo Jumanne, Novemba 26, 2024 wakati alipofunga kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilizofanyika katika viwanja vya ujenzi, Liwale Mkoani Lindi.
“Tunawaleta hawa viongozi wapigieni kura ili wakasimamie na kuendeleza yaliyomo kwenye ilani, hawa wanaweza na ndio maana tumewaleta mbele yenu, viongozi hawa ni muhimu kwasababu watawaunganisha na viongozi wa serikali, sina mashaka na wagombea wetu”
Amesema kuwa kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mafanikio makubwa yamepatikana kwa kuzingatia matarajio ya wananchi kwenye sekta za afya, elimu, maji, kilimo, uvuvi, mifugo, miundombinu, nishati na mawasiliano.
Ameongeza kuwa Serikali ya CCM chini ya Mwenyekiti Dkt. Samia kwa kutambua umuhimu wa sekta ya miundombinu, inakamilisha taratibu za ujenzi wa Barabara ya ya Masasi – Nachingwea – Liwale (175km) kwa kiwango cha lami.
Wakizungumza katika mkutano huo, wagombea wa nafasi za Uenyekiti wa vijiji, vitongoji na wajumbe wa Serikali za vijiji wamewataka wananchi kuwachagua wagombea wote wanaowakilisha CCM katika uchaguzi huo kwakuwa wana uwezo na nia ya dhati ya kusaidiana nao kuleta maendeleo.