Kijana Baraka Jumanne Maseke (21) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Nyeruma, wilayani Bunda, mkoani Mara, amejeruhiwa vibaya na mamba ndani ya ziwa Victoria, katika kijiji cha Kasahunga kilichoko wilayani humo. Habari zilizoifikia Jambo TV zinadai kwamba siku ya jana Machi 6, 2025 majira ya alfajiri, Maseke na wenzake walifika ziwani kwa ajili ya kuoga kama sehemu ya maandalizi ya kwenda shuleni.
Wakiwa ndani ya maji bila kutarajia uwepo wa mamba katika eneo hilo ambalo wanafunzi hao pamoja na wananchi wengine wa kijiji hicho wamekuwa wakilitumia kuoga na shughuli nyingine za kijamii, ghafla Maseke aling’atwa na mamba huyo eneo la ubavuni mwa mwili wake. Katika kujaribu kujinasua, aling’atwa tena mkono wake wa kulia haki iliyosababisha kijana huyo kupiga kelele kwa nguvu zaidi ili kuomba msaada kwa wenzie. Kufuatia kelele hizo, rafiki yake Maseke aitwaye Dotto Eliabu Maingu, ambaye pia ni mwanafunzi mwenzake, alijawa na ujasiri mkubwa na kumrukia mamba huyo mgongoni ili kumwokoa mwenzake. Hatua hiyo iliyomfanya mambo kuhisi hali ya hatari na kulazimika kumwachia Maseke akiwa tayari ameshamjeruhi vibaya.
Maseke alikimbizwa katika kituo cha afya cha Kasahunga ambapo katika uchunguzi wa awali wa kitabibu aligundulika kuvunjika na kusagika mfupa wa mkono wake wa kulia eneo la ubavu wa kulia pia. Hata hivyo Maseke alipewa rufaa ya kwenda kwenye hospitali ya mkoa wa Mara, iitwayo Mwl Julius Nyerere iliyoko nje kidogo ya mji wa Musoma eneo la Kwangwa. Mpaka sasa kijana huyo anaendelea na matibabu.
Tatizo la mamba na viboko katika jimbo la Mwibara wilayani Bunda, limekuwa kero kubwa kwa wananchi wa eneo hilo. Mwezi Januari, 2024, mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Kulwa Mafwimbo (46) mkazi wa kijiji cha Buzimbwe, kata ya Butimba wilayani humo, alijeruhiwa na mamba usiku wakati yeye na wenzake wakiendelea na shughuli za uvuvi. Hata kabla ya kufariki kwa Kulwa, wananchi wengine walikuwa wameshapoteza maisha katika kijiji hicho kutoka na kuliwa na mamba na hata baada ya yake matukio hayo ya kusikitisha yaliendelea.
Mkuu wa wilaya ya Bunda aliyepita Dr Vincent Naano, aliwahi kufika katika kijiji cha Buzimbwe na kutoa ahadi ya kuwavuna mamba hao kwa kushirikiana na mamlaka ya uhifadhi wa wanyamapori (TAWA). Hata hivyo tatizo hilo bado limeendelea kuwa kero kubwa kwa wananchi wa maeneo ya mwambao wa ziwa hilo kuanzia eneo la Guta mpaka Kisorya. Maeneo mengine ambayo wananchi wake wamekuwa waathirika wakubwa wa kuuawa na mamba ni pamoja na Kasuguti, Nyamitwebili, Kasahunga, Kibara, Nambaza na Kisorya.