Latest Posts

MARUFUKU MADUKA YA DAWA MUHIMU KUTOA MATIBABU

 

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekemea na kupiga marufuku kitendo cha baadhi ya maduka ya dawa muhimu kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa kinyume cha sheria.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja Mamlaka Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki, Sophia Mzirai wakati wa ufunguzi wa semina ya wadau wa maduka ya dawa muhimu kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza yenye lengo la Kujadili changamoto mbalimbali ambazo TMDA wanakumbana nazo wakati wa udhibiti wa usalama, ubora na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi katika maduka hayo.

“Katika kaguzi mbalimbali ambazo tumekuwa tukizifanya kwenye maduka hayo baadhi yamekuwa yakitoa matibabu kinyume na utaratibu mfano utakuta wanapima HIV, wanachoma sindano, wanafanya tohara, na wengine wanadiriki kuweka wagonjwa mapumziko,” amesema.

Mzirai amesema kwa kushirikiana na Baraza la Famasi mbali na kuwachukulia hatua mbalimbali kwa mujibu wa sheria ya TMDA sura ya 219 pamoja na Sheria ya Baraza la Famasi sura 113 bado changamoto hizo zimekuwa zikijirudia hali iliyopelekea kuandaa semina hiyo

“Pamoja na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria lakini katika kaguzi mbalimbali changamoto hizi zimekuwa zikijirudia unakuta wakati mwingine wanauza dawa za Serikali ndio maana siku ya leo tumeona tujadili changamoto hizi kubwa tunazokutana nazo katika kaguzi tunazozifanya katika maduka yao,” amesema

Ameongeza kuwa “Lakini vilevile tunatambua pengine na wenyewe wanachangamoto zao kwa pamoja tuweze kupata ufumbuzi wake kwa sababu lengo kuu la udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi ni kulinda afya ya jamii,” amesema Mzirai

Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dk Gabriel Mashauri amewataka wamiliki wa maduka ya dawa muhimu kutoa huduma kwa mujibu wa leseni zao ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea kutokana na ukiukwaji huo.

“Rai yetu siku zote Serikali kupitia Baraza la Famasi na TMDA na wadau wengine ni kwamba taratibu na miongozo iliyowekwa ya utoaji wa dawa kulingana na hadhi ya duka la dawa ufuatwe na kitendo cha mtu kutoka maabara na vipimo kwenda kwenye duka la dawa moja moja anamruka daktari nacho sio sahihi kwa sababu daktari ni mtu aliyesomea magonjwa kuyatibu,” amesema Dk Mashauri

Akizungumzia hoja ya kutoa huduma ya matibabu kinyume cha sheria mmiliki na mtoa huduma Duka la dawa muhimu, Happness Benjamin amesema wakati mwingine wanalazimika kutoa huduma ya kwanza kwa wagonjwa hasa maeneo ya vijijini kutokana na huduma za afya kuwa mbali

“Tunakiuka kwa sababu ni changamoto ambazo tunakuwa tunazipata kwa mfano huduma za afya zinakuwa mbali kama hospitali maeneo ya vijijini hali inayopelekea upatikanaji wa dawa na kuvifikia vituo vya afya unakuwa mgumu hali inayotulazimu wakati mwingine kumfanyia huduma ya kwanza mgonjwa ili mtu asije atasababisha kifo au madhara mengine,” amesema

Kwa upande wake mmiliki wa duka la dawa muhimu, Crianus Riacus ametoa wito kwa Serikali kuiangalia upya na kuona namna ya kuifanyia marekebisho sheria zinazowabana watoa huduma na wamiliki wa maduka hali inayopelekea baadhi yao kuvunja sheria na taratibu.

“Ukiangalia utoaji wa dawa kwenye jamii sawa ni huduma kwa jamii lakini pia ni biashara inategemea pamoja na mtoa dawa au mmiliki apate faida lakini ukija kuangalia kwenye hizo ofisi kuna mirorongo mingi ya tozo, kodi hali inayopelekea watu kwenda mbali zaidi mpaka kujikuta wakivunja sheria za nchi kulingana na uendeshaji kwa sababu Sheria zinatubana sana,” amesema Riacus

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!