Latest Posts

MASHABIKI WA YANGA NA SIMBA GEITA WATAMBIANA KUELEKEA DABI YA KARIAKOO

Kuelekea mchezo wa Dabi ya Kariakoo kati ya Simba SC na Yanga SC unaotarajiwa kuchezwa Machi 8, 2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, mashabiki wa timu hizo kutoka mkoani Geita wametambiana vikali, kila mmoja akiamini timu yake itaibuka na ushindi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali ya mji wa Geita, mashabiki wa Yanga SC wameonyesha kujiamini, wakisema kikosi chao kimekamilika na kiko tayari kuwapa burudani mashabiki wao kwa ushindi mnono. Hussein Makubi Mwananyanzala, mmoja wa mashabiki maarufu wa Yanga Geita, amesema timu yake itapata ushindi wa mabao matano kama zawadi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Mashabiki wengine wa Yanga SC waliotoa maoni yao ni Juma Maziku na Emmanuel Kazimoto, ambao walisisitiza kuwa ubora wa kikosi chao ni dhamana tosha ya ushindi katika mchezo huo mkubwa wa watani wa jadi.

Kwa upande mwingine, mashabiki wa Simba SC nao wamejibu mapigo wakisisitiza kuwa timu yao iko tayari kwa ushindi. Mabula Emmanuel, Saimon Pius, na Samwel Moleli wamesema kikosi cha Simba SC kimeimarika na kipo tayari kukabiliana na Yanga SC kwa ushindi wa kishindo.

Saimon Pius naye aliongeza kwa kusema kuwa Simba SC imefanya maandalizi ya kutosha na haitatoa nafasi kwa Yanga SC kupata ushindi kirahisi.

Mchezo huu wa Dabi ya Kariakoo unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na historia ya upinzani wa jadi kati ya klabu hizi mbili kongwe nchini Tanzania. Mashabiki wa pande zote wanaendelea kusubiri kwa hamu pambano hilo ambalo linatarajiwa kuwa na msisimko mkubwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!