Israel imeshambulia eneo karibu na mji wa Baalbek mashariki mwa Lebanon na kusababisha vifo vya watu 19, wakiwemo wanawake wanane, kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya afya ya Lebanon.
Shirika la habari la BBC limeripoti kuwa mashambulizi haya yametokea saa chache tu baada ya mamia ya maelfu ya watu kuamriwa kuondoka maeneo yao kufuatia maagizo ya jeshi la Israel.
Kwa mujibu wa meya wa Baalbek, Mustafa al-Shell, zaidi ya mashambulizi 20 yalifanyika Jumatano mchana katika eneo hilo, huku matano yakitokea ndani ya mji wa Baalbek, ambao una jengo la kale la hekalu la Kirumi linalolindwa na Unesco. Jeshi la Israel limeripoti kwamba limevamia vituo vya amri na miundombinu ya Hezbollah katika Baalbek na Nabatiyeh, kusini mwa Lebanon.
Israel pia imeeleza kuwa mashambulizi hayo yameelekezwa kwa vituo vya mafuta vya Hezbollah katika Bonde la Bekaa, ambalo linajumuisha eneo la Baalbek. Ingawa halikutoa maelezo zaidi, shirika la habari la serikali ya Lebanon lilisema matanki ya mafuta ya dizeli yalilengwa katika mji wa Douris, ambako Meya Shell alieleza kuwa picha zilionesha moshi mzito mweusi ukipanda angani.
Wakati huohuo, katibu mkuu mpya wa Hezbollah, Naim Qassem, ametangaza kuwa kundi hilo litaendeleza mpango wake wa vita dhidi ya Israel na haitaomba kusitishwa kwa mapigano. Qassem ameeleza kuwa atafuata mwelekeo wa mtangulizi wake, Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa katika shambulio la anga la Israel mjini Beirut mwezi uliopita.