Wanaharakati wanne wa kisiasa nchini Burkina Faso kutoka vuguvugu la kisiasa la Servir et Non Se Servir (SENS) wametekwa nyara, kundi lao limetangaza Jumapili.
Utekaji huo unafuatia ule wa mwanachama mwingine wa kundi hilo, mwandishi wa habari Idrissa Barry, aliyetekwa Jumanne karibu na mji mkuu, Ouagadougou. Matukio haya yanaongeza idadi ya watu waliotekwa nyara kwa kuwa wakosoaji wa utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
“Jumamosi Machi 22, wanachama wengine wanne wa kamati ya uratibu ya kitaifa, akiwemo kina mama wawili, walitekwa nyara na kupelekwa mahali pasipojulikana,” ilisema taarifa ya kundi hilo.
Vuguvugu la SENS lilikuwa limekosoa video zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita, zikionesha miili ya watu waliouawa kwa njia ya kikatili huku mikono na miguu yao ikiwa imefungwa. Wengi wa waliouawa walionekana kuwa wanawake, watoto au wazee.
Video moja ilionesha wanaume waliokuwa wamejihami kwa bunduki na visu vilivyokuwa na damu, wakiwa wamevaa fulana zinazoashiria kuwa sehemu ya vikundi vya ulinzi vya kiraia.
Serikali ya Burkina Faso imekanusha madai kuwa wanajeshi wake na wanamgambo washirika wamehusika na mauaji hayo ya halaiki.
Kwa zaidi ya muongo mmoja, Burkina Faso imekuwa ikikumbwa na machafuko yanayolaumiwa kwa makundi ya kijihadi yaliyosambaa kutoka Mali na Niger. Nchi hizo tatu zimekumbwa na mapinduzi ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni, ambapo watawala wa kijeshi wameapa kupambana na makundi hayo ya kigaidi.
Tangu mwaka 2015, ghasia nchini Burkina Faso zimegharimu maisha ya watu zaidi ya 26,000, wakiwemo raia na wanajeshi, kwa mujibu wa kituo cha kufuatilia migogoro cha ACLED.
Mwezi Februari, shirika la Observatory for the Protection of Human Rights Defenders liliituhumu serikali ya Burkina Faso kwa kutumia “utekaji nyara, kifungo haramu, upoteaji wa kulazimishwa na mateso” ili kuwanyamazisha wakosoaji wa utawala wa kijeshi.