Na Josea Sinkala, Songwe.
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Vwawa mkoani Songwe Mchungaji Amoni Mwashitete amesema Serikali kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi CCM wanaogopa uchaguzi ndio maana wanagoma kuruhusu chaguzi za huru na haki.
Mchungaji Mwashitete amesema hayo wakati wa mahojiano yake maalumu kuhusu kampeni yao ya No reforms no election na namna wanavyotekeleza kampeni hiyo kuelekea uchaguzi mkuu baadaye Oktoba 2025.
Amesema CHADEMA imedhamiria kutoa elimu ya uraia kwa wananchi kuelewa maana halisi ya mifumo ya kiuchaguzi inavyotumiwa na kunufaisha baadhi ya watu hasa walio kwenye mfumo wa Serikali akidai mifumo mingi ya kiuchaguzi inakipendelea Chama Cha Mapinduzi.
Sanjari na hayo kiongozi huyo amesema Taifa linateseka na masuala ya ukatili, mauaji, utekaji na ukandamizaji haki mbalimbali za raia pamoja na kufujwa kwa fedha za umma bila udhibiti na hatua zozote kuchukuliwa badala yake nguvu ya Serikali na vyombo vya dola vinaelekezwa kudhibiti wapinzani kama ilivyokuwa kwenye usikilizwaji wa shauri la uhaini na usambazaji taarifa za uongo dhidi ya mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Tundu Lissu akisema watu wengi walipigwa na kunyanyaswa na vyombo vya dola (Jeshi la Polisi).
Amesema Serikali inagoma kufanya marekebisho ya sheria na kanuni za uchaguzi kwasababu inajua Chama Cha Mapinduzi kitaondolewa madarakani kwasababu kimeshindwa kuwatumikia wananchi na kusisitiza kwamba mabadiliko hayo yasipofanyika basi uchaguzi mkuu wa mwaka huu utazuiwa kupitia nguvu ya Umma.
Pamoja na hayo amekemea kundi linalojulikana kwa jina la G55 linalopinga kampeni ya No reforms no election akiwashauri kuwa ikiwa hawaridhiki na maamuzi ya CHADEMA Taifa basi wako huru kuhamia vyama vingine vinavyoona na kuafiki kuingia kwenye uchaguzi mkuu licha ya kukubali kuwa hakuna sheria bora na tume huru ya uchaguzi, tume ambayo ameikosoa vikali kuwa haina uhuru wowote kwasababu inateuliwa na makada wa CCM badala ya kuundwa na watu huru.