Rais wa Marekani, Joe Biden, na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wamefanya mazungumzo ya simu yaliyotarajiwa kwa muda wa dakika 30. Hii inasadikiwa kuwa ni mawasiliano yao ya kwanza tangu mwezi Agosti, ambapo walijadili hatua za Israel kulipiza kisasi kwa shambulio la kombora lililofanywa na Iran wiki iliyopita.
Â
Kwa mujibu wa Ikulu ya White House, mazungumzo hayo yalikuwa ya moja kwa moja na yenye tija, na viongozi hao wawili wamekubaliana kuwasiliana mara kwa mara katika siku zijazo. Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, pia alishiriki katika mazungumzo hayo.
Â
Wakati huohuo, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, alitangaza kuwa mashambulizi dhidi ya Iran yatakuwa mabaya, sahihi, na zaidi ya yote, ya kushangaza.
Â
Mazungumzo haya yanaakisi msuguano kati ya malengo mawili makuu: Kwa upande mmoja, Biden anahofia Marekani kujikuta ikijihusisha kwenye vita na Iran, vita vinavyoweza kuwa hatari na visivyo na ulazima. Kwa upande mwingine, baadhi ya viongozi wa Israel wanaona fursa ya kusababisha pigo kubwa dhidi ya adui yao mkubwa, Iran.
Â
Nchini Israel, mafanikio ya kijeshi dhidi ya Hezbollah huko Lebanon yamewapa nguvu baadhi ya Waisrael wanaotaka kukabiliana vikali na Iran.
Â
Hata hivyo, licha ya mashambulizi dhidi ya Gaza ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 42,000, wakiwemo raia wengi, Netanyahu hajafanikiwa kufikia malengo yake ya kusambaratisha Hamas au kuwaokoa mateka waliotekwa nyara. Hadi sasa, karibu mateka 100 bado wanashikiliwa, huku wengi wakihofiwa kuwa wamefariki.
Â
Uharibifu uliofanywa dhidi ya maadui wa Israel, yaani Hezbollah na Hamas, umesababisha baadhi ya Waisrael kuamini kuwa hatua zaidi zinahitajika, ikiwemo shambulio la moja kwa moja dhidi ya Iran. Waisrael wengi wanavutiwa na wazo la kufanya shambulio la anga dhidi ya maeneo ya Iran, yakiwemo vituo vya nyuklia vilivyojificha kwenye milima, ambavyo wanahisi vinaweza kutumika kutengeneza bomu la nyuklia.