Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameihimiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mkoani Mtwara kumsimamia kwa ukaribu muwekezaji anayefanya shughuli za usafirishaji wa makaa ya mawe kupitia bandari hiyo kuhakikisha analeta vifaa vinavyohitajika ili kudhibiti vumbi linalosababishwa na makaa ya mawe.
Waziri huyo ametoa wito huo wakati wa ziara ya kukagua utendaji wa bandari ya Mtwara na eneo la Kisiwa Mgao, litakalojengwa bandari maalum kwa ajili ya kusafirisha mizigo michafu kama makaa ya mawe na saruji.
Prof. Mbarawa amesema kuwa hatua za kudhibiti vumbi la makaa ya mawe ni muhimu ili kuepusha athari kwa shughuli za maendeleo za wananchi wanaoishi karibu na bandari hiyo.
“Ni muhimu kwa muwekezaji kuleta vifaa vya kisasa vya kudhibiti vumbi ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi bila madhara yoyote,” amesema Waziri Mbarawa.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Saidi Nyengedi, ameeleza jinsi vumbi la makaa ya mawe limeathiri maisha ya wananchi na kusababisha kufungwa kwa viwanda kama kiwanda cha ubanguaji wa korosho, ambacho kiliajiri zaidi ya wafanyakazi 400.
Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa amewataka wafanyakazi wa bandari hiyo kuongeza kasi na ufanisi katika kuhudumia meli ili kuepusha meli kutumia muda mrefu bandarini, jambo ambalo linaweza kusababisha hasara kwa uchumi wa taifa.
Serikali imepanga kujenga bandari mpya katika eneo la Kisiwa Mgao kwa ajili ya kusafirisha mizigo michafu kama sehemu ya kuboresha huduma za bandari na kupunguza athari za vumbi kwa maeneo ya makazi. Bandari hiyo inatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto za sasa na pia kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Mtwara.