Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, mkoani Geita, Nicodemas Maganga, amewataka wananchi kutokubali kutishwa na mtu yeyote na kusimama kidete kuunga mkono viongozi wanaotokana na Wilaya hiyo badala ya kuchagua wageni ambao baadaye huwatupa na kushindwa kuwahudumia.
Maganga aliyasema hayo wakati wa mkutano wake na wananchi wa Kata ya Ngemo, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wakazi wa Mbogwe kutambua kuwa wilaya yao ina wasomi na vijana mahiri kisiasa, wenye uwezo wa kuwaongoza.
“Suala la kuchagua viongozi kutoka nje ya wilaya wenye tamaa ya madaraka ni kukaribisha watu wasiokuwa sahihi, ambao wanaweza kushindwa kushughulikia kero za wananchi,” alisema Maganga.
Mbunge huyo aliwahimiza wananchi kuwa wazalendo kwa kuunga mkono viongozi wa eneo lao, akisema ni njia pekee ya kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana katika wilaya hiyo.