Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Oran Manasse Njeza, ameshiriki mazishi ya Yoramu Uled Jilla, baba mzazi wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Vijijini, Lameck Jilla, aliyefariki dunia Desemba 11, 2024.
Mazishi hayo yamefanyika katika makaburi ya familia kijijini Isuto, Kata ya Isuto, Tarafa ya Isangati, na yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali.
Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi, Njeza amewataka wananchi kuendelea kuishi kwa imani na tumaini kwa Mungu huku wakifanya kazi kwa bidii, akisisitiza kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya “Kazi Iendelee.” Pia amewapongeza wananchi wa Mbeya Vijijini kwa kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na utulivu, akiwahimiza kudumisha amani hiyo ili kuimarisha maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini, Akimu Sebastian Mwalupindi, ametoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, akibainisha mchango mkubwa wa familia hiyo katika uongozi wa Chama Cha Mapinduzi. Amesema marehemu Yoramu Jilla alikuwa kiongozi wa chama ngazi ya tawi, huku mtoto wake, Lameck Jilla, akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi Wilaya ya Mbeya Vijijini, na mjukuu wake, Yusuph Lameck Jilla, akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Kata ya Isuto.
“Familia ya marehemu Mzee Jilla ni baraka kwa Chama Cha Mapinduzi. Kwa kizazi chake, tumeona jinsi walivyotuletea viongozi waliodhamiria kuleta maendeleo kwa wananchi kupitia Serikali ya CCM,” amesema Mwalupindi.
Aidha, Mwalupindi amewashukuru wananchi wa Mbeya Vijijini na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla kwa kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na mshikamano, akiwataka kuendelea kulinda umoja uliopo kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.
Mazishi hayo yamewakutanisha viongozi wa chama na serikali, wananchi wa kijiji cha Isuto, na wadau mbalimbali wa maendeleo, wakionesha mshikamano wa hali ya juu kwa familia ya marehemu Yoramu Jilla.