Latest Posts

MCHENGERWA ABARIKI UJENZI SHULE YA LWANJILO MBEYA DC

Na Josea Sinkala, Mbeya

Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohammed Mchengerwa, ameweka jiwe la msingi majengo manne ya shule mpya ya sekondari Lwanjilo Halmashauri ya wilaya ya Mbeya kwa ajili ya kuanzisha masomo ya kidato cha tano na sita kwenye shule hiyo ambayo imeanza miaka miwili iliyopita.

Waziri Mchengerwa ameeleza hayo wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Mbeya vijijini na viongozi mbalimbali katika shule ya sekondari Lwanjilo wilayani Mbeya kwenye uwekaji jiwe la msingi majengo ya vyumba vinne vya madarasa pamoja na mabweni mawili ya shule hiyo kwa ajili ya kidato cha tano na sita.

Amesema Serikali ya awamu ya sita ina malengo mema na wananchi wake wote kuhakikisha wanapata huduma rafiki katika maeneo yao katika sekta mbalimbali ikiwemo kwenye elimu.

Pamoja na kuweka jiwe la msingi majengo hayo, ameielekeza Halmashauri ya wilaya ya Mbeya kupitia kwa mkurugenzi mtendaji wake bi. Erica Yegella kuhakikisha wanamalizia ukamilishaji miundombinu ya shule hiyo ili kuanza kwa kidato cha tano na kuahidi Serikali kuu kutowaangusha.

Diwani wa kata ya Lwanjilo Mhe. Adamu Lugano Mwakamalisya, ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika kata yake na kuomba shule hiyo mpya ifikishiwe huduma ya maji ili kuwasaidia wanafunzi na wananchi wa Lwanjilo, ombi ambalo Waziri Mchengerwa ameahidi kulifikisha kwa Waziri wa maji Mhe. Juma Aweso kuhakikisha maji yanafika kijijini hapo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya Erica Yegella, amesema ujenzi wa shule hiyo ni kutokana na fedha kutoka Serikalini kuu ambapo kwa mwendelezo wa majengo manne kuelekea kuanzisha kidato cha tano na sita zaidi ya shilingi million mia nne zimetumika.

Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Mbeya amemhakikishia Waziri wa TAMISEMI kuwa matarajio yao ni kukamilisha mradi wa ujenzi huo hivi karibuni.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais (TAMISEMI) Mhe. Mohammed Omary Mchengerwa, amefanya ziara ya siku moja mkoani Mbeya ambako ametembelea Halmashauri za jiji la Mbeya, Halmashauri ya wilaya ya Mbeya na Chunya akizindua na kuweka mawe ya msingi miradi mbalimbali ya maendeleo sanjari na kuzungumza na wananchi akisisitiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na Serikali yao ili kufikia maendeleo endelevu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!