Latest Posts

MCHINJITA: KUSUSIA UCHAGUZI SIO SULUHISHO, AZIMIO LA TABORA LINASEMA TUSHIRIKI

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, amesema kuwa Azimio la Tabora juu ya Kura Tatu ni ushahidi wa wazi kuwa kususia uchaguzi si njia mufti katika mapambano dhidi ya utawala kandamizi.

Akihutubia wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Julai 1, 2025, huko Kalinzi, Jimbo la Kigoma Kaskazini, Mchinjita amesema kuwa wakati wa utawala wa kikoloni, haki ya kuchagua na kuchaguliwa ilidhibitiwa kwa kiwango cha kutisha, huku masharti ya kibaguzi kama kupiga kura tatu yakiwekwa ili kudhoofisha ushiriki wa Watanganyika.

“Wapo waliopendekeza kususia uchaguzi hadi mfumo bora wa kidemokrasia uwekwe, lakini wazee wetu walitumia busara ya hali ya juu. Walitambua kuwa mapambano hayawezi kushindwa kwa kususa. Walijua kwamba mabadiliko hayataletwa kwa kususia bali kwa kushiriki na kushindana,” alisema Mchinjita huku akishangiliwa na wananchi waliokusanyika kwenye uwanja wa mkutano.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa uzoefu wa Azimio la Tabora unapaswa kuwa somo kwa kizazi cha sasa kinachoandaa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. “Tuna wajibu wa kuendeleza mapambano kwa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huu. Tusiruhusu hofu au vizingiti vituvunje moyo. Muhimu ni kulinda kura kwa nguvu zetu zote.”

Hotuba ya Mchinjita imepokelewa kwa hisia kali mitandaoni, huku wachambuzi wa siasa wakisema inachochea ari mpya ya kizalendo na kujitoa kwa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia.

Mkutano huo wa Kalinzi ni sehemu ya mikutano ya hadhara ya chama hicho inayoendelea nchi nzima kwa ajili ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!