Mchungaji mmoja nchini Kenya aliyetambuliwa kwa jina la Daniel Mururu anachunguzwa kutokana na tuhuma za ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa polisi.
Uchunguzi huu umeibuka baada ya hasira za wakazi, ambao walichoma moto kanisa lililoendeshwa na Mururu katika kaunti ya Meru mwishoni mwa mwezi uliopita.
Mururu, kiongozi wa Kanisa la Pentekoste la Afrika Mashariki, anashutumiwa pamoja na wazee wa kanisa na washemasi wake kwa kushiriki katika vitendo vya udhalilishaji. Tuhuma hizi zinajumuisha kuwavua nguo wanawake, kuacha wanawake wakiwa uchi, kuwaondolea nywele sehemu za siri, na kuwa na mahusiano ya kimapenzi nao, kulingana na ripoti ya polisi iliyotolewa Jumatatu.

Ripoti hiyo inasema kuwa zaidi ya wanawake na wasichana saba wenye umri wa miaka 17 hadi 70 wanadaiwa kuwa wahanga wa vitendo hivi vya ukatili, ikiwa ni pamoja na msichana wa shule mwenye umri wa miaka 17 aliyepewa ujauzito.
Uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kwamba Mururu alikuwa akiendesha dhehebu lenye msimamo mkali, ambapo wafuasi walishawishiwa kufanya vitendo vya udhalilishaji kwa hofu ya kuathirika na magonjwa au utasa ikiwa watakaidi maagizo ya mchungaji.
Kenya, nchi yenye idadi kubwa ya waumini wa kikristo, imekuwa ikijitahidi kudhibiti makanisa na madhehebu yasiyo na uadilifu yanayojihusisha na uhalifu.
Katika moja ya matukio yaliyovuta hisia za dunia, ni lile la Mchungaji Paul Mackenzie kukamatwa mwezi Aprili mwaka jana baada ya miili kugundulika katika makaburi ya watu wengi. Waokoaji walitumia miezi mingi kutafuta maiti kutoka kwenye eneo la vichaka karibu na mji wa Malindi, ambapo jumla ya miili 448 zimefukuliwa.
Uchunguzi wa maiti umeonesha kuwa wengi walifariki kwa njaa, lakini baadhi, ikiwa ni pamoja na watoto, walionekana kuuliwa kwa kunyongwa, kupigwa, au kukosa hewa.
Sakata la mauaji haya, linalojulikana kama “mauaji ya msitu wa Shakahola,” limechochea wito kutoka kwa serikali kwa udhibiti mkali wa madhehebu nchini.
Tume iliyoanzishwa na Rais William Ruto kuchunguza vifo hivyo na kupitia sheria za mashirika ya kidini ilikamilisha ripoti yake mwezi Julai, ikitoa mapendekezo ya usimamizi wa serikali.