Latest Posts

MDEMU: WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUFIKISHA TAARIFA ZA KIZAZI CHENYE USAWA

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bi. Felister Mdemu, amefungua kikao kazi cha kujenga uelewa kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu Programu ya Kitaifa ya Kizazi Chenye Usawa, leo Jumanne Juni 3, 2025, jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimeilenga kuwajengea uwezo Wahariri katika kuhariri na kusanifu taarifa kuhusu utekelezaji wa programu hiyo kabla ya kuifikisha kwa umma kupitia vyombo vya habari.

Akizungumza katika ufunguzi, Mdemu amesema kuwa Serikali inatambua nafasi kubwa ya vyombo vya habari katika kuhamasisha usawa wa kijinsia, hasa katika eneo la haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake.

Amesema, “Vyombo vya habari ni wadau wakubwa wa kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa.”

Ameeleza kuwa Programu hiyo ya miaka mitano (2021/22–2025/26) inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni matokeo ya ushiriki wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa lililofanyika Paris, Ufaransa mwaka 2022.

Mdemu amebainisha kuwa utekelezaji wa programu hiyo unajikita katika maeneo manne muhimu: uwekezaji wa kijinsia katika huduma za matunzo, kazi zenye staha kwa wanawake, upatikanaji na umiliki wa rasilimali za uzalishaji, na mipango ya uchumi inayozingatia jinsia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Jukwaa la Kizazi chenye Usawa, Mhe. Angellah Kairuki (MB), amesema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana, ikiwemo kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, upatikanaji wa mikopo kupitia asilimia 10 za mapato ya Halmashauri, na ujumuishaji wa wanawake katika mipango ya maendeleo.

Alisema,

“Leo wanawake wanamiliki ardhi, wanahusika katika uongozi wa vyama vya ushirika, na bajeti nyingi sasa zina mrengo wa kijinsia.”

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma, kushawishi sera, na kubadili mitazamo ya kijamii.

Akizungumza kwa niaba ya UN Women, Naibu Mwakilishi Mkazi nchini Tanzania, Katherine Gifford, amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa katika kutekeleza ajenda ya usawa wa kijinsia kupitia Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa.

Amesema “Wahariri ni walinzi wa simulizi, wachoraji wa taswira ya taifa. Mna jukumu la kuifanya ajenda ya kizazi chenye usawa kuwa ya kweli kwa kila Mtanzania.”

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, jamii, sekta binafsi na vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya kuleta mabadiliko ya kweli ya kijamii na kiuchumi kwa wanawake na wasichana.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesisitiza kuwa kikao hicho ni fursa muhimu kwa wahariri kuelewa kwa kina Programu ya Kizazi Chenye Usawa ili waweze kuandika na kuripoti kwa weledi na ufanisi kuhusu masuala ya haki na usawa wa kijinsia.

“Tunayo matarajio kwamba Wahariri wakishafahamu mpango huu basi lile kusudio la kuwa na kizazi chenye usawa linatimizwa,” alisema Balile huku akieleza kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kusukuma mbele ajenda ya kijinsia nchini.

Balile amehimiza umuhimu wa kujenga matumaini kwa Watanzania kupitia habari zenye kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, akisema,

“Tuliangalie taifa letu na tujenge matumaini kwa Watanzania. Usawa wa kiuchumi ni wa msingi kwa maendeleo jumuishi ya taifa letu.”

Programu ya Kizazi Chenye Usawa inatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar, kwa ushirikiano wa serikali, UN Women, na wadau wengine wa maendeleo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ahadi za Kitaifa katika Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!