Na Helena Magabe – Tarime
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Tarime, Mhandisi Masinino Swalo, amesema kuwa mitaa 13 ya Tarime Mji imeingizwa katika mpango wa kuunganishiwa umeme, na taratibu za utekelezaji zinaendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Machi 25, 2025, Eng. Swalo alieleza kuwa mitaa itakayopata umeme katika awamu hii ni ile iliyopo karibu na miundombinu mikubwa ya umeme. Kwa mitaa ambayo bado haina miundombinu hiyo, itahusishwa katika awamu zijazo, kwani kuna mchakato wa upatikanaji wa line kubwa za umeme.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, kati ya mitaa 81 inayounda Tarime Mji, mitaa 68 tayari ina umeme. Changamoto kwa mitaa iliyosalia ni upatikanaji wa line kubwa za kusafirisha umeme, lakini juhudi zinaendelea kuhakikisha inapata huduma hiyo kwa awamu.
Aidha, Eng. Swalo alieleza kuwa Serikali imelenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwisho wa mwaka 2025, kila kijiji nchini kinakuwa na umeme. Kwa sasa, juhudi zimeelekezwa katika kuhakikisha mitaa na vitongoji navyo vinaunganishiwa umeme. Hadi sasa, mitaa 52 imeingizwa katika mpango huo na mkandarasi tayari ameanza kazi.
Hata hivyo, alieleza kuwa bado kuna changamoto ya wizi wa nyaya za shaba (copper) na mita kutoka kwenye transfoma, jambo linalosababisha usumbufu kwa wananchi. Alisema kuwa hali hii inachangiwa na baadhi ya vijana waliopata elimu ya umeme lakini wakakosa ajira, hivyo kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu.