Latest Posts

MENEJA TARURA: SHERIA YETU YA BARABARA NI KALI, INA FAINI NA KIFUNGO

 

Na Helena Magabe, Tarime

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Tarime, Charles Marwa, amesema kuwa Sheria ya Barabara ya TARURA ni kali kwani inatoa adhabu ya faini isiyozidi shilingi 300,000 au kifungo kisichozidi mwaka mmoja kwa yeyote atakayekutwa na kosa. Kulingana na aina ya kosa, mhusika anaweza kulipa faini, kutumikia kifungo, au kupatiwa adhabu zote kwa pamoja.

Akizungumza na Jambo TV leo Machi 25, 2025, ofisini kwake, Marwa alifafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007, kifungu cha 49 na 50 vinaeleza makosa na adhabu zinazohusiana na sheria hiyo. Alisema kuwa mifugo inayotembea bila uangalizi barabarani, inayofungwa ndani au karibu na barabara, au inayotembea katikati ya barabara, inaweza kukamatwa kwa mujibu wa sheria hiyo.

Marwa alibainisha kuwa mifugo ni moja ya chanzo cha ajali na uharibifu wa barabara zinazotengenezwa kwa gharama kubwa. Aliongeza kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliitisha kikao kilichohusisha watendaji wa kata na mitaa, wenyeviti wa mitaa, maafisa wa misitu na mazingira, wafugaji, pamoja na TARURA, ambapo kila taasisi ilielezea majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu kuwekwa kwa alama za vivuko vya mifugo kwenye barabara za TARURA, Marwa alisema bado hazijawekwa. Alifafanua kuwa viongozi wa wafugaji walikubaliana kufanya mazungumzo na wafugaji ili wachague maeneo yanayofaa kisha wawasilishe mapendekezo yao ifikapo Machi 24, 2025. Hata hivyo, mpaka sasa hawajawasilisha mapendekezo hayo.

“Waliuliza maswali mengi, wakahoji wanapopeleka ng’ombe mnadani au malishoni, je, wawabebe kichwani? Yote niliyatolea majibu Niliwaeleza kuwa wanapovusha mifugo yao barabarani wanapaswa kuwa makini. Walipendekeza wawekewe alama za vivuko na maeneo maalum ya kulishia mifugo. Nikawaambia hilo ni sahihi, lakini siwezi kutenga maeneo pasipo wao kuyapendekeza Tulikubaliana waanishe na kuwasilisha maeneo wanayoyaona yanafaa ili TARURA yapitishe, lakini mpaka sasa hawajaleta mapendekezo,” alisema Marwa.

Katika operesheni ya Machi 22, 2025, maafisa wa mazingira na misitu walikamata ng’ombe 33 waliokuwa wakichungwa katika maeneo mawili tofauti wawili kwenye uwanja wa wazi mkabala na nyumbani kwa DC Gowele,mmoja alikutwa kwa nyuma Wamiliki wa mifugo hiyo ni Kinyunyi Mtogori, Chacha Masero, na Ibrahimu Range ambao walitakiwa kulipa faini ya shilingi 200,000 kwa kila ng’ombe, jumla ikitakiwa shilingi 6,600,000. Hata hivyo, walifanikiwa kulipa shilingi 1,700,000 tu.

Ni baada ya kumwomba msamaha Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele, machi 23,2025 ambaye aliwapunguzia faini na kuwataka walipe shilingi 50,000 kwa kila ng’ombe. Hivyo ng’ombe hao walirejeshwa Machi 23, 2025, kwa Wafugaji hao baada ya malipo hayo kufanyika.

Akizungumza na Jambo TV kwa njia ya simu machi 22,2025 Meja Gowele alisema kuwa wafugaji wamezuiwa kuchunga mifugo yao katika barabara zote za TARURA na TANROADS ili kulinda miundombinu ya barabara.

“Tumemaliza kupanda miti 10,000 jana tu, lakini leo tunakuta ng’ombe wanachungwa maeneo hayo. Wafugaji wanapaswa kuelewa kuwa mifugo haipaswi kuwa mijini. Wewe ni mwandishi unaelewa , tusaidie kufikisha ujumbe huu,” alisema Meja Gowele.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!