Jeshi la Polisi nchini limewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kutii sheria bila shuruti na kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu na vitendo vyote vinavyotishia amani katika jamii.
Wito huo umetolewa na Mrakibu wa Polisi Dkt. Ezekiel Kyogo kutoka Kamisheni ya Polisi Jamii Makao Makuu ya Dodoma, alipokuwa akitoa elimu ya usalama kwa wakazi wa mtaa wa Nyantorotoro, Manispaa ya Geita, mkoani Geita.
Hikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa programu maalum ya kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wa serikali za mitaa, inayofadhiliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), kupitia kampeni ya Community Policing Outreach inayoongozwa na kaulimbiu isemayo “Polisi Jamii, ni Wajibu Wetu Sote.”
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Elisante Ulomi, kutoka Kamisheni hiyo hiyo, amewataka wananchi kutozifumbia macho dalili za uhalifu, akisisitiza kuwa uhalifu hauna mipaka na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa anayevunja amani .
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyantorotoro, Jonas Faida, ameushukuru mgodi wa GGML na Jeshi la Polisi kwa kuwaleta elimu hiyo muhimu, akisema kuwa ushirikiano baina ya wananchi na vyombo vya usalama ni njia bora ya kulinda amani katika jamii.
Programu hii inatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine ya Mkoa wa Geita, ikiwa na lengo la kuimarisha uhusiano kati ya polisi na wananchi, pamoja na kujenga jamii inayokataa vitendo vyote vya kihalifu.