Latest Posts

MIKOPO CHECHEFU INAVYODIDIMIZA KASI YA UKUAJI WA UCHUMI NCHINI

Ndoto na matamanio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona Watanzania wanakopeshwa mikopo nafuu yenye riba chini ya asilimia 10 ili waweze kujiimarisha kiuchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla wake, hata hivyo inaelezwa kuwa ndoto hiyo inakuwa ngumu kufikiwa kutokana na wafanyabiashara wachache kujitajirisha isivyo halali kupitia mikopo wanayokopa katika mabenki kadhaa ndani na nje ya nchi kisha kukataa kulipa na hivyo kuzifanya taasisi za fedha kujihami kwa kuweka riba kubwa na masharti magumu ili kulinda mitaji yao kukwepa kile kinachoitwa ‘mikopo chechefu’

Ni kutokana na sababu hiyo ya uwepo wa ‘mikopo chechefu’ ambayo wakopaji hukopa mabilioni ya pesa na kukataa kulipa kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo kukimbilia Mahakamani na kushinda kesi kiujanja ujanja, ndipo sasa pamezaliwa aina mpya ya mikopo inayowatesa mamilioni ya Watanzania maarufu kama ‘mikopo kausha damu’ inayozidi kushamiri kila kona nchini na kila uchao

Hii ni mikopo inayotajwa kuongoza kuwafilisi wananchi hasa wa vipato vya chini ikiwemo watumishi wa serikali na binafsi kutokana na riba kuwa kubwa inayotolewa kirahisi bila ya masharti mengi hivyo kuvutia watu wengi kuikimbilia ambapo unaweza ukakopa milioni moja ukalipa milioni kumi kama ‘utani’

Taarifa zinaonyesha kuwa urahisi wa upatikanaji wa mikopo hii ndio unaowaponza wakopaji ambapo mteja anaweza kujaza fomu saa nane mchana, dakika chache baadae akakopeshwa, na huku akiambiwa riba ni ndogo kumbe kila milioni moja anayochukua ina riba yake, baadaye kuangalia anajikuta anatakiwa kulipa mamilioni ya pesa ambayo kiuhalisia hawezi kulipa deni lote, na riba huanza kupanda kila mwezi, uchunguzi unaonyesha kuwa ni kutokana na kushamiri kwa ‘mikopo chechefu’ ndiko kunakopelekea kuongezeka kwa mikopo inayoumiza ambayo hufanywa na taasisi ama watu binafsi wanaokuwa kimbilio la wananchi wasio na uwezo wa kupenya kwenye mikopo rasmi ya kibenki

“Kama tunaambiwa mfanyabiashara mmoja tu amekopa zaidi ya bilioni 100 na akakataa kulipa, huyo ni mmoja tu, hebu jiulize ni wajasiliamali wangapi wa aina yangu na wenye mitaji isiyozidi milioni 5, au mama lishe wangapi, au wamachinga wangapi wangeweza kukopeshwa hizo bilioni 100 zilizokaliwa na mtu mmoja bila huruma?, unaona lile guta pale? (anaonyesha pikipiki ya matairi matatu) unayaona yanavyopiga kazi?, na unaona vijana walivyoyachangamkia kubeba mizigo hapa Kariakoo kutumia maguta?, sasa yale yanauzwa milioni kama tano hivi, jiulize sasa bilioni 100 unaweza nunua mangapi kama yale na yangeweza kutoa ajira kiasi gani, muda mwingine hizi benki zipunguze kushobokea matajiri, sisi wapiganaji tupo huku na nakuhakikishia hakuna mtu angeweza kushindwa kurejesha mikopo ya maguta kama yale maana mzigo wa kubeba upo kila siku, hapo sijazungumzia Bodaboda ambazo ni chini ya milioni 3 kila moja, kwa mabilioni hayo tungejiajiri Watanzania wangapi, achana na hawa wauza madafu, wauza kahawa na watembeza bidhaa nyinginezo ambao mitaji yao haifiki hata laki tano, tungejiajiri wangapi?, kuna haja sasa ya serikali kuangalia upya vipaumbele vya namna ya ukopeshaji, bila hivyo tutaendelea kukimbilia ‘kausha damu’ tu hakuna namna nyingine’’ -Joshua Mwaibage, mfanyabiashara mdogo, soko la kimataifa la Kariakoo, Dar es Salaam

Naye, John Sembuyu ambaye ni mchambuzi na mtaalam wa masuala ya uchumi akitolea maoni amesema ni ndoto kwa jambo hilo kutokea kwa mazingira ya sasa ikiwa jitihada mahsusi hazitachukuliwa kudhibiti hali hiyo, “uchumi wa kibenki una vipimo vyake, kadri kasi ya mikopo isiyolipika inavyozidi kuongezeka, ndivyo urahisi wa mabenki kukopesha unazidi kupungua, lazima benki zijihami kukwepa kuingia mtego wa BOT (Benki Kuu ya Tanzania) unaozuia kiwango cha mikopo isiyolipika kuvuka asilimia 5 ya mikopo yote, kwa mantiki hiyo lazima benki zikomae na riba kubwa na masharti magumu ili kujihakikishia usalama wa pesa zake’’

Itakumbukwa kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) amewahi kutoa tangazo la kuwataka Watanzania kutoa taarifa kwa benki hiyo juu ya wafanyabiashara wanaojihusisha na utoaji wa mikopo bila kuwa na leseni za kufanya hivyo kama wanavyotakiwa na kifungu cha 17 cha sheria za huduma ndogo za fedha 2018, hata hivyo inaonekana utekelezaji wa jambo hilo umekuwa mgumu kutokana na ukweli kuwa uwezo wa wananchi kuifikia benki hiyo na kuchambua kwa kutambua kama anayewakopesha ni taasisi iliyosajiliwa ama haijasajiliwa ni mdogo sana

Aidha, hali ya wananchi wengi wanaojikuta wanaingia na kuangukia kwenye taasisi zinazokopesha mikopo kwa riba kubwa haziwaruhusu hata kufikiria mara mbili kipindi wanataka kukopa kwani wengi wao hukimbilia kukopa kama chaguo la mwisho baada ya kukwama kwa majaribio yao mengi hasa kushindwa kukopeshwa benki, taarifa zaidi kuhusu jambo hilo zinadai kuwa sio ananchi wasio wafanyakazi tu ndio wanateseka na aina hii ya mikopo lakini pia hata watumishi wa serikali hasa wafanyakazi wapya wanaoanza maisha mapya kazini hukutana na aina hii ya mikopo kutokana kuwa na uhitaji mkubwa wa kupata fedha za kujikimu na kuanzishia maisha kabla ya kupokea mshahara na hivyo kujikuta wanaangukia mikononi mwa wakopeshaji hawa, Idadi ya vijana walioanza kazi na wanaoshuhudia mishahara yao inapita kwenda kulipa mikopo hii ni kubwa na inasikitisha kwani kutokana na kukithiri kwa mikopo hii kunawafanya watumishi hao kukosa hamu ya kufanya kazi

“Hata sisi wafanyakazi wa serikali tunapambana nayo mikopo ya namna hiyo, vijana wengi sana wanaoanza kazi wanateseka na mikopo hiyo, yupo kijana mmoja alikopa milioni 8, mpaka sasa amerejesha milioni 21 na bado mkopo haujaisha, kwa kifupi ni hatari, tamko tu la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ama Waziri kuwa watu watoe taarifa juu ya uwepo wa mikopo ama taasisi za hivi wala halitoshi, wakopaji hukimbilia huko baada ya kubanwa sana, serikali kupitia BOT lazima watafute suluhu ya uhakika hasa kupitia mabenki, lazima tujue ni kwanini kuna ugumu kwa mabenki kutoa mikopo yenye unafuu wa masharti kiasi cha watu kukimbilia ‘kausha damu’ maana kama benki zingekuwa zinatoa mikopo bila shida nina hakika hii ‘kausha damu’ isingekuwepo’’ -ni sehemu ya yale aliyozungumza mmoja wa wafanyakazi wa serikali ambaye jina lake limehifadhiwa ambaye ni miongoni wa wanaoumizwa na mikopo ‘kausha damu’

Uzoefu unaonyesha kuwa mikopo ‘kausha damu’ ipo ya aina mbalimbali mingineyo ikihusisha hadi taasisi zilizosajiliwa kisheria lakini wanaweka vipengele vigumu katika mikataba yao hasa utata wa uchakataji wa riba na hivyo kuwatesa wakopaji kulipa, huko nyuma imewahi kutaarifiwa kuwa serikali imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kuwezesha mabenki kujiendesha hususani yale mabenki inayoyamiliki, lengo likiwa ni kuona mabenki yakijiendesha kutokana na kukosa mitaji, dalili za fedha hizo kupotea ama kutafunwa na wajanja inaonekana wazi kama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hatachukua hatua za haraka kudhibiti michezo michafu ya upigaji wa fedha za mabenki hayo kupitia mikopo isiyolipika kwa makusudi

Taarifa zaidi zinadai kuwa serikali imepanga kuiwezesha Benki ya TCB (Tanzania Commecia Bank) mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 130 ili kuihuisha benki hiyo inayoundwa na mjumuiko wa benki kadhaa zilizofilisika kutokana na mikopo chechefu nchini, miongoni mwa benki zilizofilisika na kuungwa pamoja kuunda TCB ni pamoja na benki ya wanawake, benki ya Posta, Twiga Bancorp na TIB Corporate ambazo kwa nyakati tofauti benki hizo zilifilisika pamoja na mambo mengine lakini pia mikopo chechefu ikitamalaki

Aidha, serikali inaelezwa kuweka zaidi ya shilingi bilioni 100 kuhuisha mtaji wa benki ya uwekezaji TIB ili iendelee na biashara ambayo hadi sasa inasuasua kutokana na kuelekea kufilisika kwa mikopo chechefu ambayo hailipiki, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere katika taarifa yake amsema serikali inahitaji kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kukidhi mtaji wake, hii tafsiri yake ni kwamba benki hiyo ambayo kiuhalisia inajikongoja imefikia hatua hiyo kutokana na uwepo wa ‘mikopo chechefu’ kwa wafanyabiashara wakubwa walioamua kuigeuza benki hiyo kuwa shamba la bibi kwa kukopa na kukataa kulipa

Wakati wa makabidhiano ya ripoti ya mwaka wa fedha 2022/23 kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu, jijini Dodoma katika taarifa yake CAG amesema kuwa benki hiyo ina mtaji mdogo ikiwa na mtaji wa 88.12bn/- tu kinyume na matakwa ya 200bn/- kwa mujibu wa muongozo wa benki na taasisi za fedha wa mwaka 2020/21, “Benki ya Kilimo inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa mtaji, hivyo kutoa wito kwa serikali kuendelea kuingiza pesa zaidi ili kuboresha mtaji wa wakopeshaji wa kilimo”

Hata hivyo amesema anafahamu mipango ya serikali ya kuingiza 118.88bn/- ili kukuza mtaji wa wakopeshaji wa kilimo na kukidhi mahitaji ya mtaji, katika maendeleo ya hivi karibuni mwezi uliopita, serikali ilipata mikataba ya mikopo ya kimataifa kufadhili sekta ya miundombinu na kilimo, katika utaratibu huo wa mikopo, sekta ya kilimo ilipata shilingi bilioni 166.4 ili kuongeza mtaji wa TADB unaolenga kugharamia shughuli za kilimo hivyo kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kukuza biashara ya bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi pamoja na kuongeza ajira na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla

Taarifa za uhakika tulizonazo zinaonyesha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 100 za benki hiyo zipo kwa wafanyabiashara wachache waliogoma kulipa mikopo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukimbilia Mahakamani kujificha, miongoni mwa wafanyabiashara waliokopa kiasi kikubwa cha fedha katika benki hiyo ni pamoja na kampuni ya Global agency iliyochukua bilioni 26 kwa mradi wa shamba la kilimo mkoani kagera huku Chobo Investment ikichukua bilioni 12 bila kurudisha, mwingine anayetajwa kukomba mabilioni ya shilingi katika benki hiyo ni kampuni ya Kahama oil millers (KOMU) ambayo imechukua zaidi ya shilingi bilioni 40 na hadi sasa haijulikani itarejeshaje kiasi hicho cha pesa, kukithiri kwa mikopo chechefu sio tu kunayaathiri mabenki yanayotoa mikopo hiyo bali pia hupeleka athari za moja kwa moja kwa Watanzania ambao wanategemea mikopo ishuke riba ili na wao wakope

“Miongoni mwa sababu za kisayansi za riba kuwa zaidi ya asilimia 18 ni wastani wa mikopo chechefu, mikopo mingi inayoshindwa kurejeshwa inayatia mabenki hasara kubwa na kwa bahati mbaya wengi wanaoshindwa kurejesha ni wafanyabiashara wakubwa ambao hukopa mabilioni, hivyo ili benki kujilinda na hasara hizo huweka riba kubwa kufidia mapengo hayo, ni vyema serikali iendelee kuweka kanuni ngumu zinazosimamia urejeshwaji wa mikopo ili kutokuruhusu wanyonge wengi wanaotaka kukopa kujiimarisha kibiashara kukutana na vikwazo ambavyo kimsingi hawastahili kukutana navyo, wafanyabiashara wakubwa wakikopa wanakopa kweli, imagine mtu amekopa bilioni 40 halafu amekataa kulipa na akibanwa anakimbilia Mahakamani, bilioni 40 ukisema uwakopeshe mama lishe, au bodaboda, au vijana tu wa biashara za mtaji mdogo ungekopesha watu wangapi?, mkopo huo ungezalisha ajira ngapi?, mapato kiasi gani yangekusanywa? lakini wapi, anachukua mfanyabiashara mmoja, anakwenda kununua V8 anatamba nazo mjini na akipita tunamuamkia ukifika wakati wa kulipa anakimbilia Mahakamani’’ -CPA Crispin Peter, mtaalam wa masuala ya fedha.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!