
Na. Anania Kajuni
Wadau wa elimu jijini Mwanza wameipongeza Serikali kwa kutatua changamoto ya miundombinu ya kujifunzia kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Buhongwa.
Akizungumza na Jambo TV mara baada ya kutembelea shule hiyo, Afisa Elimu Watu Maalumu Awali na Msingi Jiji la Mwanza, Zakia Ahmed, amesema hapo awali shule ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mabweni, upungufu wa vyumba vya madarasa, ukosefu wa vifaa wezeshi vya kujifunzia watoto wenye mahitaji maalumu, pamoja na ukosefu wa uzio wa shule.
“Hapo mwanzo, shule hii haikuwa na bweni hata moja kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, lakini sasa tumejengewa mabweni mawili yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 160. Hali hii imewezesha shule kupokea watoto zaidi ya 100 wanaoendelea kupata huduma bure chini ya usimamizi wa walimu na walezi wao,” amesema.
“Awali, tulikuwa na darasa moja tu la wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ambalo tulipata ufadhili kutoka Shirika la Kijapani la KOICA. Lakini katika kipindi kifupi, tumefanikiwa kujenga madarasa manne, hivyo kufikia madarasa matano,” ameongeza Zakia.
Hata hivyo, afisa elimu huyo amesema kuwa shule bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa walimu kutokana na idadi kubwa ya watoto wanaoendelea kuletwa na wazazi, hivyo kuiomba Serikali kuongeza walimu wa elimu maalumu katika Jiji la Mwanza.
“Changamoto tuliyonayo ni upungufu wa walimu. Wanafunzi ni wengi na kila mmoja ana aina yake ya ulemavu, hivyo tunahitaji Serikali kutuletea walimu wapya. Hadi sasa tuna walimu wanane, lakini uhitaji ni walimu zaidi ya 20, kulingana na mahitaji ya wanafunzi. Kwa mfano, mtoto mwenye usonji anapaswa kuwa na mwalimu mmoja, wakati kwa wanafunzi wenye matatizo ya afya ya akili, mwalimu mmoja anatakiwa kuwahudumia wanafunzi watano,” amesema Zakia.
Ameongeza kuwa, “Kutokana na upungufu huu, mwalimu mmoja analazimika kuwahudumia wanafunzi zaidi ya 30, hali inayosababisha changamoto kubwa. Hili si tatizo la shule hii pekee, bali pia katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuna baadhi ya vitengo vyenye watoto 40 lakini walimu ni wawili tu. Tunaomba Serikali itusaidie kuongeza walimu wa elimu maalumu.”
Mkazi wa Nyegezi, Josbeli Sikazwe, ambaye ni mzazi wa mtoto mwenye ulemavu anayesoma katika Shule ya Msingi Buhongwa, amesema kuwa licha ya kuboreshwa kwa miundombinu ya shule, bado changamoto ya upungufu wa walimu inabaki kuwa kikwazo.
“Maendeleo ya taaluma ni mazuri, lakini tatizo kubwa ni uhaba wa walimu. Watoto ni wengi, madarasa yamejengwa, lakini walimu ni wachache. Kwa mfano, mwanangu hakuwa na uwezo wa kusoma wala kuandika, lakini sasa anaweza, jambo linalonihamasisha kuendelea kumleta shuleni,” amesema Sikazwe.
Mkazi mwingine wa Mkolani, Imejenga Stevin, ambaye pia ni mzazi wa mtoto mwenye usonji, ameipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu ya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu, hali iliyowahamasisha wazazi kuwapeleka watoto wao shule.
“Natoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kutujali sisi wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalumu. Hapa Buhongwa huduma ni nzuri, walimu wanajitahidi sana kufundisha. Zamani wanafunzi walikuwa wachache, lakini sasa watoto wengi wanapelekwa shuleni kutokana na maboresho yaliyofanyika,” amesema Stevin.
Akimwakilisha Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buhongwa, Mwalimu Phelister Ndegeulaya, ameipongeza Serikali kwa kutoa zaidi ya Shilingi milioni 486 katika kipindi cha miaka miwili ili kuboresha miundombinu ya shule, jambo linalochochea ujifunzaji na ufundishaji.
“Nashukuru sana Serikali ya Rais Samia. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 na mwaka huu wa 2024/2025, tumepokea jumla ya Shilingi milioni 486.3, zilizotumika kujenga mabweni mawili kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu – wavulana na wasichana – ambapo kila bweni linachukua wanafunzi 80,” amesema.
“Pia tumejengewa vyumba vinne vya madarasa, vyoo, pamoja na uzio wa shule ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi. Tunaishukuru Serikali kwa mchango wake mkubwa, hasa katika vifaa wezeshi vinavyosaidia kufundishia wanafunzi wenye mahitaji maalumu,” ameongeza Mwalimu Ndegeulaya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalumu katika shule hiyo, Sasi Nzololo, amesema maboresho hayo yamewahamasisha wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni, kwani hapo awali walikuwa na wanafunzi wachache, lakini sasa idadi imeongezeka.
“Hapo awali tulikuwa na wanafunzi wachache, wasiozidi 10, lakini sasa tuna wanafunzi 192. Hii ni kutokana na juhudi za Serikali kuboresha miundombinu chini ya Rais Samia. Tunamshukuru sana,” amesema Nzololo.
Ameongeza kuwa, “Tunampongeza pia Afisa Elimu Zakia Ahmed kwa jitihada zake kubwa za kuhakikisha elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu inasonga mbele. Hivi sasa tuna wanafunzi wanaoishi bweni na wengine wanaotokea nyumbani, ilhali hapo awali wote walikuwa wanatokea nyumbani.”
Mwanafunzi wa darasa la sita, Kelvin Nkama, amepongeza Serikali kwa ujenzi wa uzio wa shule, akisema kuwa umesaidia kupunguza ajali za kugongwa na vyombo vya moto.
“Kabla ya kuwekwa uzio, watoto walikuwa wakitoka nje na kuzurura, hali iliyosababisha ajali nyingi. Wengine walifariki kutokana na kugongwa na vyombo vya moto, jambo lililowafanya wazazi wengi kutoleta watoto wao shuleni. Sasa hali ni salama zaidi,” amesema Nkama.
Mwanafunzi mwingine wa darasa la sita, Anna Emmanuel, ameomba Serikali kuwaongezea madawati, kuboresha vyoo, na kununua gari la shule ili kurahisisha usafiri kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanaotoka nyumbani.
“Tunashukuru kwa maboresho haya, lakini bado tunaomba madawati zaidi, vyoo vya kisasa, na gari la shule kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wenye ulemavu kufika shuleni kwa urahisi,” amesema Anna.