Halmashauri ya mji wa Njombe kwa kushirikiana na uongozi wa serikali za vijiji na mitaa umeendelea na jitihada za kuhakikisha vijiji na mitaa inakuwa na ofisi za kisasa ili kuepuka mali na nyaraka za serikali kukaa mitaani.
Kutokana na jitihada hizo,kikao cha Maendeleo ya kata (KAMAKA) kata ya Njombe mjini, kimeagiza mitaa yote ya kata hiyo kuhakikisha inakuwa na ofisi za kisasa ifikapo 2030.
“Kata ya Njombe ni lazima tuwe na ofisi za kisasa,kuna mitaa tayari wana ofisi na wengine kwenye ujenzi wako hatua ya mbele zaidi kwa hiyo tumekubaliana 2025-2030 mitaa yote iwe na ofisi”amesema Alatanga Nyagawa Diwani kata ya Njombe Mjini.
Ennocy Lupimo ni Mtendaji wa kata ya Njombe mjini anasema mji wa Njombe unachangamoto kubwa kwenye upatikanaji wa maeneo lakini wamekuwa na mkakati wa kutoa fidia kwa watu wenye maeneo ili waweze kupisha ujenzi huku akitaka mitaa kujisimamia kwa kuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo amekuwa akitoa fedha za ndani kukamilisha ujenzi.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kata ya Njombe Mjini yenye wakazi 37900 ina mitaa tisa,ambapo mitaa sita mpaka sasa tayari ina ofisi huku mitaa mingine ikiendelee na jitihada za ujenzi ili kurahisisha shughuli za ufanyaji kazi kwenye mitaa.