Latest Posts

MJUE MWALIMU MKUU ALIYEFANIKIWA KUNUNUA MASHINE MBILI ZA PHOTOCOPY

 

Na Helena Magabe – Tarime

Mwalimu Daniel Meli ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mazoezi Buhemba ambaye ana ndoto ya kuibadilisha shule hiyo na kuiweka kwenye historia ya kuwa miongoni mwa shule bora na za mfano katika Wilaya ya Tarime na hata Mkoa wa Mara. Akiwa na dhamira hiyo, Mwalimu Meli amefanikisha ununuzi wa mashine mbili za photocopy; ya kwanza akiwa Shule ya Msingi Mtahuru na ya pili sasa akiwa Buhemba.

Akiwa Mtahuru, Mwalimu Meli alitumia mbinu ya kuhamasisha wadau mbalimbali wakiwemo wachimbaji na wamiliki wa mashimo ya dhahabu katika mgodi wa Kibaga, uliopo karibu na shule hiyo. Kupitia michango yao pamoja na baadhi ya wazazi, alifanikiwa kununua mashine ya kwanza ya photocopy na kuokoa gharama za kuchapisha mitihani mara kwa mara.

Alipohamia Buhemba, zoezi la kuchangisha fedha lilikuwa gumu zaidi, ingawa kila mzazi alitakiwa kuchangia shilingi 3,000. Hata hivyo, hakukata tamaa. Alijitahidi kuhamasisha wazazi na hatimaye mnamo Aprili 2, 2025, alifanikiwa kununua mashine ya pili ya photocopy yenye thamani ya shilingi 2,500,000. Mashine hiyo ilizinduliwa rasmi mbele ya wazazi wa wanafunzi wa darasa la saba Aprili 24, 2025.

Mwalimu Meli alisema wanafunzi zaidi ya 800 kati ya 1,476 ndio waliochangia, na akatumia nafasi hiyo kuwashukuru wazazi wote waliotoa mchango wao. Aliwahimiza kuendeleza mshikamano kwa maendeleo ya shule akisema, “Maendeleo yanahitaji nguvu, akili, fedha na muda.”

Alieleza kuwa moja ya mbinu za kuinua ufaulu ni vikao baina ya walimu na wazazi, mitihani ya ushirika, majaribio ya mara kwa mara na wanafunzi kusoma limidio kwa bidii. Ameongeza kuwa wiki ijayo anatarajia kuwapeleka wanafunzi wa darasa la saba kufanya mtihani wa ushirika katika Shule ya Msingi Turwa, ikiwa ni hatua ya kwanza ya kujipima. Pia, wamepanga kuendelea kufanya mitihani ya ushirika hata nje ya Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na walimu wa wilaya na mikoa mbalimbali.

Katika uzinduzi huo, viongozi kutoka Halmashauri ya Mji waliipongeza shule hiyo kwa hatua hiyo ya maendeleo. Afisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, Bi. Jaina Ibrahimu Meena, alisema ingawa mwanzo wazazi waliona ugumu kuchangia shilingi 3,000, sasa wameona matunda ya juhudi hizo.

Aliongeza kuwa Buhemba ni miongoni mwa shule 18 kati ya 39 katika Halmashauri ya Mji ambazo zinatarajiwa kupokea vifaa vya kidijitali. Pia, ni miongoni mwa shule tatu (pamoja na Turwa na Mtahuru) zinazohudumia watoto wenye mahitaji maalum. Watoto hao wana fursa ya kusoma chuo cha FDC Tarime bure kwa miaka miwili, wakihitimu kidato cha kwanza hadi cha nne kwa miaka miwili.

Afisa Elimu Taaluma Msingi, Bw. Ryoba Mariba, aliwataka wazazi kutenga muda kwa ajili ya watoto wao tangu wakiwa wadogo. Alisisitiza kuwa maendeleo ya mtoto hayapaswi kusubiri hadi awe mkubwa. Aliongeza kuwa shule inaweza kufanikisha ufaulu wa wanafunzi wote, kama ilivyowahi kutokea shule moja jijini Dar es Salaam iliyofaulisha wanafunzi wote 1,400.

Mzazi Wankyo Marwa aliomba wanafunzi watoro na wakorofi wanaochangiwa na wazazi wao wafuatiliwe ipasavyo. Naye mzazi Hilda John alishauri kuwa walimu wasiwafukuze wanafunzi nyumbani kwa madai ya pesa ya limidio kabla ya mwezi kuisha; badala yake walipwe hadi mwisho wa mwezi, ndipo hatua zichukuliwe kwa wanafunzi wasiolipa.

Mzazi mwingine, Charles Daudi Mahongija, aliwaomba wazazi waendelee kuwaamini walimu, kwani wanajitahidi kwa juhudi kubwa kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi. Alihimiza wazazi kuchangia kila hitaji la shule bila kusita kwa ajili ya maslahi ya watoto wao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!