Latest Posts

MKUTANO WA G20 WAANZA AFRIKA KUSINI, MAREKANI YAKATAA KUSHIRIKI

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa tajiri duniani (G20) umeanza leo nchini Afrika Kusini, lakini Marekani imesusia mkutano huo, hatua inayoongeza mvutano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa mujibu wa BBC, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alitangaza mapema mwezi huu kupitia mitandao ya kijamii kuwa hatohudhuria mkutano huo, akieleza kuwa “Afrika Kusini inafanya mambo ya kutamausha.” Rubio alisisitiza kuwa jukumu lake ni kulinda maslahi ya Wamarekani na kuhakikisha kodi zao hazitumiki vibaya.

Uamuzi wa Marekani unakuja wakati uhusiano kati ya Washington na Pretoria ukiendelea kudorora, hasa baada ya Rais Donald Trump kutangaza kusitisha misaada kwa Afrika Kusini. Hatua hiyo ilichukuliwa kama jibu kwa muswada wa ardhi uliotiwa saini hivi karibuni, ambao unaruhusu serikali ya Afrika Kusini kutwaa ardhi bila fidia katika mazingira fulani.

Hata hivyo, Pretoria imekanusha mara kwa mara kwamba hakuna unyakuzi holela wa ardhi au mali ya kibinafsi, ikisisitiza kuwa mageuzi ya ardhi ni hatua muhimu kwa usawa wa kijamii na kiuchumi nchini humo.

Mkutano huu wa G20 ni wa kwanza wa mawaziri wa mambo ya nje tangu Afrika Kusini ilipochukua nafasi ya urais wa kundi hilo mwezi Desemba mwaka jana. Serikali ya Afrika Kusini ilitarajia kutumia mkutano huu kukuza masuala muhimu kwa nchi zinazoendelea, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha za maendeleo na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, kutokuwepo kwa Marekani kunaweza kuathiri mafanikio ya mkutano huo, hasa kwa kuwa Marekani ina ushawishi mkubwa ndani ya G20 na kwenye masuala ya uchumi wa kimataifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!