Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza mitaani nchini Uturuki baada ya Ekrem Imamoglu, meya wa Istanbul na mpinzani mkuu wa Rais Recep Tayyip Erdogan, kukamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma za ufisadi.
Imamoglu, aliyekuwa akitarajiwa kuwania urais kwa tiketi ya chama cha Republican People’s Party (CHP) katika uchaguzi wa 2028, alikamatwa kabla ya kutangazwa rasmi kama mgombea wa upinzani siku ya Jumapili.
Baada ya kukamatwa kwake, maandamano makubwa yalizuka usiku wa kuamkia leo, ambapo vikosi vya usalama vilitumia mabomu ya machozi, risasi za mpira, na maji ya kuwasha kujaribu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakikusanyika jijini Istanbul.
Imamoglu alitumia mtandao wake wa kijamii wa X kueleza msimamo wake kabla ya kuzuiliwa rumande, akisema “Sitatetereka.”. Rais Erdogan ameshutumu vikali maandamano hayo, akilaumu chama cha CHP kwa kujaribu “kuchochea ghasia na kugawanya watu.”
Mke wa Imamoglu, Dilek Kaya, aliwahutubia waandamanaji na kusema kuwa udhalimu dhidi ya mumewe umevuka mipaka.
Takwimu za mamlaka za Uturuki zinaonesha kuwa zaidi ya watu 700 wamekamatwa tangu maandamano hayo yaanze.
Chama cha CHP kimekuwa na ushirikiano wa kisiasa na Chama cha Usawa na Demokrasia cha Watu wa Kurdish (DEM) tangu uchaguzi wa mitaa wa mwaka jana. Hata hivyo, DEM kimehusishwa na Kurdistan Workers’ Party (PKK), kundi ambalo limepigwa marufuku Uturuki, Umoja wa Ulaya, Uingereza na Marekani kwa tuhuma za ugaidi.
Mwezi huu, PKK ilitangaza kusitisha mashambulizi yake, baada ya kuendesha uasi kwa zaidi ya miaka 40 dhidi ya serikali ya Uturuki.
Maandamano haya yanatajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea Uturuki tangu maandamano ya Gezi ya mwaka 2013, yaliyoanzia Istanbul kwa kupinga kubomolewa kwa bustani ya umma kabla ya kusambaa nchi nzima.