Latest Posts

MRADI WA MAJIKO YA GESI KUOKOA MAZINGIRA NA GHARAMA ZA MAISHA

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mradi wa kusambaza majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya 50% unaotekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ushirikiano na Kampuni ya Lake Gas.

Pongezi hizo zilitolewa Desemba 10, 2024, wakati wa utekelezaji wa mradi huo wilayani humo ambapo wananchi wamesema kuwa mradi huo umekuja wakati mwafaka kutokana na changamoto za upatikanaji wa kuni na mkaa, hasa kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Neema Rumas, mkazi wa kijiji cha Siwandeti, alisema kwamba upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kupitia gesi utawasaidia kupunguza gharama za maisha na kuokoa muda wanaotumia kutafuta kuni au mkaa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Siwandeti, Daniel Mitiweki, amebainisha kuwa mradi huo pia una mchango mkubwa katika uhifadhi wa mazingira. Amesema matumizi ya majiko ya gesi yamekuwa suluhisho la tatizo la ukataji wa miti uliokithiri katika kijiji hicho kwa ajili ya kuni na mkaa.

Msimamizi wa Mradi wa REA Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Gift Kombe, amewasisitiza wananchi kuzingatia elimu inayotolewa kuhusu matumizi sahihi ya majiko ya gesi ili kuhakikisha yanadumu na kuleta manufaa yaliyokusudiwa. Pia amewataka wananchi kuhakikisha wanajaza mitungi ya gesi mara inapoisha ili kuendeleza matumizi ya nishati safi.

Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034, uliozinduliwa Mei 2024 na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkakati huo unalenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kuboresha hali ya maisha ya wananchi, na kulinda mazingira.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!