Latest Posts

MSAADA WA KISHERIA WA MAMA SAMIA KWENDA KUTATUA MIGOGORO MOROGORO,DKT.NDUMBARO

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amewataka wakazi wa Mkoa wa Morogoro kutumia fursa ya msaada wa kisheria unaotolewa chini ya kampeni ya MAMA SAMIA kama njia ya kuleta maridhiano na kutatua migogoro inayoendelea kati ya wananchi kwani utakuwa ni daraja la amani na haki.

Dkt. Ndumbaro amesema hayo katika uzinduzi rasmi wa kampeni ya msaada wa kisheria wa MAMA SAMIA(MAMA SAMIA LEGAL AID) uliofanyika mjini Morogoro ambapo ameeleza kuwa ingawa lengo kuu la kampeni hiyo ni kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, lakini pia itaimarisha utawala wa sheria na kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wote bila kujali hali ya kifedha au kijamii.

“Serikali inatambua kuwa migogoro mingi ya kijamii, ikiwa ni pamoja na ile ya ardhi, ndoa, mirathi na mipaka, imekuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi wetu kwa hiyo, kampeni hii inakuja kama suluhisho la kisheria ambalo linatarajiwa kutoa msaada wa haraka na wa ufanisi katika maeneo haya,” Dkt. Ndumbaro.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima, amesisitiza kuwa Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa Mikoa inayohitaji msaada wa kisheria hasa kutokana na migogoro ya ardhi, migogoro ya ndoa, masuala ya mirathi na pia changamoto za mipaka kati ya jamii na vijiji.

Kyobya amefafanua kuwa huduma hii itasaidia kupunguza idadi ya migogoro inayozunguka masuala hayo, ambayo mara nyingi huwafanya wananchi kuwa na matatizo ya kisheria yanayohitaji ufumbuzi wa haraka na wa haki.

Nao baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Morogoro wameeleza furaha yao kwa kupokea huduma hiyo ya msaada wa kisheria, wamesema kuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wananchi wa kawaida bila kikwazo chochote,Wakazi hao wametaja kuwa hatua hiyo inakwenda kufungua milango ya kutatua migogoro ya familia, mirathi, na pia kuondoa mashaka yanayotokana na migogoro ya ardhi na mipaka.

Kwa upande mwingine, wadau wa kisheria wamesisitiza kuwa kampeni hii ni muhimu katika kuimarisha elimu ya kisheria kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kutoa mwanga juu ya haki zao na namna ya kuzidai.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!