Latest Posts

MSIBA WA ALI MOHAMED KIBAO: TASWIRA NA MJADALA MPANA WA HAKI NA USALAMA NCHINI

Na Amani Hamisi Mjege.

Jiji la Tanga na Tanzania kwa ujumla limegubikwa na majonzi baada ya kifo cha ghafla cha Ali Mohamed Kibao, mjumbe wa CHADEMA, ambaye alitekwa na kupoteza maisha kwa njia yenye utata.

Tukio hili limezua mijadala kuhusu haki, usalama, na ushiriki wa vyombo vya usalama nchini, huku viongozi mbalimbali wakitoa wito wa uchunguzi wa kina ili haki itendeke.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, akizungumza kwa niaba ya serikali katika msiba wa Kibao uliofanyika mkoani Tanga ameelezea huzuni ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa tukio hilo. Waziri Masauni alisema,

“Mheshimiwa Rais amehuzunishwa sana na tukio hili. Ninawaomba wananchi kuacha kushutumu, na badala yake, kama mtu ana ushahidi wa kuonesha, apeleke kwa mamlaka husika.”

Hata hivyo, kauli ya waziri huyo ilionekana kupingwa vikali na viongozi wa CHADEMA, akiwemo mwenyekiti Freeman Mbowe. Mbowe alisema kuwa, “Jamii imechoshwa na matukio haya ya utekaji na mauaji ya viongozi wa chama chetu. Tunaiomba serikali iunde tume ya kijaji kufanya uchunguzi huru juu ya kifo cha Kibao.”

Katika hotuba yake, Mbowe alisisitiza umuhimu wa tume ya kijaji akisema, “Sisi ambao tuna ushahidi hatuko tayari kutoa ushahidi wetu kwa vyombo vya polisi tunavyovituhumu. Ni lazima Rais aunde tume huru ya kijaji.”

Aliongeza kuwa CHADEMA ina ushahidi wa kutosha kuonesha wahusika wa utekaji na mauaji hayo, lakini tume huru ndiyo inayoweza kuendesha uchunguzi wa haki.

Godbless Lema, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, aliungana na wito huo akisema, “Hasira hizi ambazo zinaonekana msibani, zinaweza kuhamia barabarani kama hatua madhubuti hazitachukuliwa. Msiba huu uwe wa mwisho kwa mtu aliyeuawa kwa kutekwa.”

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo bara , Isihaka Mchinjita alidai kuwa Jeshi la Polisi limekosa uwezo wa kulinda usalama wa raia kutokana na kile alichokieleza kuwa ushuhudiwaji wa matukio ya ukatili bila majibu ya kuridhisha.

Msiba huu umeshtua jamii ya Tanga na Tanzania kwa ujumla, na familia ya marehemu imeelezea huzuni yao juu ya kifo cha ghafla cha mpendwa wao.

“Mzee wetu alikuwa mtu mwema na mnyenyekevu, hatuelewi kilichotokea,” alisema mmoja wa wanafamilia.

Msiba huu umefungua mjadala mkubwa juu ya haki na usalama wa raia nchini, na wengi wanatarajia kuona kama wito wa kuundwa kwa tume huru utafanikiwa.

Mbali na viongozi wa CHADEMA na serikali, viongozi wa dini na mashirika ya kijamii walikusanyika kutoa heshima zao kwa Ali Mohamed Kibao.

“Tumehuzunika sana kumpoteza kiongozi wetu wa Tanga,” alisema Meya wa Jiji la Tanga.

Tukio hili linazidi kuwa moto kwenye mjadala wa kitaifa kuhusu uwajibikaji wa vyombo vya dola na haki za raia, huku ikisubiriwa hatua za serikali kujibu wito wa kuundwa kwa tume huru

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!