Latest Posts

MSIMAMO WA CHADEMA LUPA, WAMTAKA LISSU, ‘SIO MHAINI’

 

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Lupa (Chunya) mkoani Mbeya, kimeeleza msimamo wake kuwa kitatekeleza kwa vitendo kampeni yake ya No reforms no election kama ilivyoelekezwa na ngazi ya Taifa kutokana na wanachodai ni kutokuwepo kwa sheria na kanuni rafiki za kiuchaguzi wakidai mwenyekiti wao sio mhaini bali ni mtetezi wa haki za binadamu hivyo hapaswi kuendelea kushikiliwa na mamlaka.

 

Hayo yameelezwa na katibu wa Chama hicho jimbo la Lupa Yohana Mpamba (Mcotton), wakati akitoa tamko la chama hicho (CHADEMA) kwa niaba ya uongozi wa Chama jimbo la Lupa kuhusu utekelezaji wa operesheni ya No reforms no election akisema Lissu amekuwa akiongoza operesheni ya kutaka maboresho au mabadiliko ya sheria za kiuchaguzi na hana makosa ya wazi kama inavyodaiwa hata kushtakiwa na kutaka mashtaka dhidi yake kuondolewa.

 

Katibu huyo wa CHADEMA jimbo la Lupa, amesema CHADEMA jimbo la Lupa inaendelea kueneza agenda hiyo kwa wanachama na wananchi kuhakikisha wnaaungana kudai kufanyika kwa maboresho ya sheria za kiuchaguzi lasivyo kuhakikisha uchaguzi mkuu baadaye Oktoba 2025 haufanyiki kwa madai kuwa sheria na kanuni za uchaguzi ni kandamizi na kwamba tume huru ya uchaguzi inaongozwa na viongozi watokanao na Chama Cha Mapinduzi ambacho ni chama tawala hivyo kuhofia kuipendelea CCM kwenye chaguzi mbalimbali kama ambavyo imekuwa ikidaiwa kwenye chaguzi kadhaa zilizopita.

 

Amesema chama hicho kiko pamoja na kiongozi wao wa Taifa Tundu Lissu (mwenyekiti wa CHADEMA Taifa) kwenye madhira anayopitia ya kushtakiwa kwa kesi ambayo inatokana na harakati zake za kudai mifumo bora ya chaguzi.

 

Kwa upande wake katibu wa Baraza la wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) jimbo la Lupa Stella Mwakasekele, ameeleza masikitiko yake kwa Serikali anayosema ndio chanzo cha kuvurugwa kwa chaguzi za Tanzania kuingiliwa na vyombo vya dola, kuwepo kwa upendeleo kwa Chama Cha Mapinduzi akisema upendeleo huo unatokana na sheria, kanuni na taratibu kutokuwa rafiki kwa vyama vya upinzani.

 

Baadhi ya wanachama waliohojiwa mjini Chunya wamesema hawako tayari kuingia kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu pasipo kufanyika kwa maboresho/marekebisho ya sheria za uchaguzi kisha kuendelea kupigania agenda mama ambayo ni upatikanaji katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!