Wahudumu wa afya katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wametakiwa kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa pamoja na kuzingatia usafi kuanzia kwenye sakafu mpaka vifaa vinavyotumika kuhudumia wagonjwa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa tiba mbalimbali kwenye kituo cha afya Ufukoni kilichopo kwenye Manispaa hiyo, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini Hassan Mtenga amewasisitiza wahudumu hao kutunza vifaa hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu pamoja na kuzingatia usafi huo.
Pia amemtaka Mkurugenzi na Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo kushirikiana kwa pamoja kutoa elimu kwa jamii kuhusu huduma ya kujifungua ili kuepusha malalamiko ya wananchi yanayojitokeza, kuwa wanatozwa pesa wakati wa kujifungua.
“Niseme Mkurugenzi, mimi nawaambia hawa madiwani tuelimishe jamii kwasababu swala la uzazi liko tofauti kwenye uzazi sio kila uzazi utakuwa ni bure hapana uko uzazi mwingine unahitaji gharama na hizi gharama lazima zigharamiwe. Kuna wa kujifungua bure ila pamoja na kujifungua bure ila kuna aina ya kujifungua, DMO hata asubuhi kuwepo na darasa wagonjwa wakija awepo mwalimu wa kuwapa elimu” Ameeleza Mtenga.
Aidha Mganga Mfawidhi wa Kituoa hicho, Dkt. Christ Nzali amesema hapo awali kulikuwa na upungufu wa vifaa tiba ambavyo vilipelekea wagonjwa wa kupumzishwa kuwa wachache hivyo kupitia vifaa hivyo idadi ya wagonjwa wa kupumzishwa itaongezeka.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwalimu Nyange amemuomba mbunge huyo kuendelea kupambana ili katika mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri iweze kupata kituo kingine cha afya kwenye maeneo ambayo yako mbali na mji ambako kuna uhitaji na wingi wa watu.
Vifaa vilivyotolewa vina thamani ya shilingi milioni 7.60 vikijumuisha magodoro 15, seti ya vifaa vya kujifungulia 10, makabati 15, vitanda vya hospitali 15 na shuka 60.