Barua za vitisho zilizosambazwa na watu wasiojulikana zimesababisha taharuki kubwa katika ofisi mbalimbali za kata ya Ruhuhu, wilayani Ludewa, mkoani Njombe.
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Kings FM, barua hizo ziliripotiwa kubandikwa usiku wa kuamkia Desemba 3, 2024, kwenye ofisi za viongozi wa kijiji, kata, na vyama vya siasa.
Miongoni mwa ofisi zilizolengwa ni Ofisi ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngelelenge ambapo barua iliyoandikwa ilisema, “marufuku kuingia humu maana hatukukuchagua!”. Kwa upande wa ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Ngelelenge, barua ilisomeka, “na wewe Mtendaji wa Kijiji ukitaka kuingia humu jikane nafsi yako ndipo uingie humu!”.
Barua nyingine ilielekezwa Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Ruhuhu ikisema, “umetuibia sana tumechoka kuvumilia. Sasa hivi tunakwambia kutembea kwako mwisho saa 12 jioni jihadhari muda huo. ulipo upo na sisi mda wote, utakachokipata utakijua mwenyewe.”.
Katika ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), barua ilisema, “tumevumilia tumechoka madude yenu mnayofanya. tunaomba mtupishe, hata sisi vijana tupo hapa na tunaweza kuongoza”.
Kwa upande mwingine katika ofisi ya chama cha ACT Wazalendo, mambo yalikuwa tofauti kwani barua ilisomeka, “tunaomba endeleeni kukaza hivyohivyo. Msipokaza, mkalegeza tutawaweka kwenye kundi moja la wale wajinga tuliowaandikia barua.”
Akizungumza na kituo hicho cha habari, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngelelenge, Joseph Mapunda (CCM), ambaye alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa kijiji wa Novemba 27, 2024, amethibitisha kupokea vitisho hivyo. Amesema kuwa tangu barua hizo ziwekwe, hajaweza kufungua ofisi yake kutokana na hofu ya usalama wake, na tayari amewasiliana na viongozi wa chama chake pamoja na Jeshi la Polisi ili wachukue hatua dhidi ya vitisho hivyo.