Mahakama ya Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya imemuhukumu kutumikia adhabu ya kifungo bcha maisha jela Anthony Anosisye Mwangaka [53] mkazi wa Mbugani Wilayani Chunya baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka na kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 09.
Kwa mujibu wa jeshi la Polisi mkoani Mbeya, hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Chunya James Mhanusi kwenye shauri lililokuwa likiendeshwa na mwendesha mashtaka wa Serikali wakili Mwajabu Tengeneza.
Kwa mujibu wa taarifa na maelezo ya upande wa mashtaka mbele ya mahakama hiyo, Mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 17, 2024 katika kijiji cha Mbugani Wilayani Chunya na kukamatwa Desemba 22, 2024 kisha kufikishwa mahakamani ambapo ametiwa hatiani kwa makosa mawili ya kubaka na kulawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 09.
Jamuhuri ilidai wakati wa uwasilishaji maelezo yake kuwa mama mzazi wa mhanga alibaini tukio hilo wakati akifua nguo za ndani za mtoto wake baada ya kukuta zimechafuka na alipomchunguza mtoto wake ndipo alibaini kunajisiwa na Anthony Anosisye Mwangaka.
Wakati huohuo Mahakama hiyo imemhukumu kifungo cha maisha gerezani Said Kombo Kandonga [60] mkazi wa kibaoni Wilayani Chunya baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 08.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Chunya James Mhanusi na Mwendesha mashitaka wa Serikali wakili Mwajabu Tengeneza ambapo mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 16, 2024 katika Kijiji cha Kibaoni Wilayani Chunya na alikamatwa Oktoba 02, 2024 na kufikishwa mahakamani kujibu shtaka hilo ambapo amekutwa na hatia kwa kosa la kumnajisi (kumbaka) mtoto huyo.
Polisi inaendelea kuhimiza wananchi kuacha tabia ya kujihusisha na matendo ya uhalifu na tamaa ya kutaka kupata fedha kwa njia za mkato na njia ovu badala yake wafanye kazi halali ili kuendesha maisha yao lasivyo watakamatwa na sheria itachukua mkondo wake hivyo kugharimu maisha yao na kuleta hasara kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.