Latest Posts

NAIBU RAIS WA KENYA: WABUNGE WANAHONGWA ILI KUPANGA KURA YA KUNIONDOA MADARAKANI

Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amefichua madai mazito kuhusu njama za kumwondoa madarakani kupitia kura ya kutokuwa na imani naye, baada ya kudai kuwa baadhi ya Wabunge wanahongwa na kutishwa ili kuanzisha hoja ya kumwondoa ofisini.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Citizen TV ya Kenya usiku wa Ijumaa, Gachagua alieleza kuwa mikutano ya siri imekuwa ikifanyika usiku katika maeneo ya Nyahururu na Kitisuru, kwenye nyumba ya Waziri wa Baraza la Mawaziri, kwa lengo la kupanga njama hizo.

Bila kutaja majina ya wahusika, Gachagua alidai kuwa Wabunge walipokea hongo katika mikutano hiyo, akieleza kuwa wengi wao walilazimishwa kukubaliana na masharti yaliyowekwa.

“Mimi hupata taarifa nyingi, na unapowaita watu kwenye mkutano ukidhani kuwa ni siri kubwa… tunapata taarifa hizi wakati mikutano inaendelea,” alisema Gachagua.

“Mikutano imefanyika Nyahururu, mikutano pia imefanyika Kitisuru kwenye nyumba ya Waziri wa Baraza la Mawaziri, tunajua kilichokuwa kikijadiliwa. Tunajua kiasi cha fedha kilichohamishwa. Tunajua haya mambo,” aliongeza Naibu Rais.

Mkutano uliofanyika Nyahururu wiki hii ulihudhuriwa na zaidi ya Wabunge 69 ambao walimchagua Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki, kama kiongozi wao wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya, hatua ambayo ilimpuuza Gachagua. Hatua hiyo imepewa jina la “Azimio la Nyahururu.”

Aidha, taarifa zinaonesha kuwa mkutano mwingine ulifanyika hivi karibuni kwenye nyumba ya Waziri wa Baraza la Mawaziri, ambapo Wabunge 21 walikubaliana kumvua madaraka Naibu Rais Gachagua, wakimshutumu kwa kukiuka katiba na tabia mbovu. Hata hivyo, Gachagua aliondoa wasiwasi juu ya mgawanyiko katika eneo la Mlima Kenya, akisisitiza kuwa anaungwa mkono na wananchi.

“Yeyote mwenye tatizo na uongozi wangu au mwenendo wangu ana kila sababu ya kuzungumza na mwajiri wangu. Hawa ndio watu wanaoweza kupima utendaji wangu,” alisema Gachagua.

Alieleza pia kuwa uhusiano wake na wanasiasa wengine umekuwa na changamoto kutokana na ukweli wake wa kusema mambo bila kuficha.

“Kila mtu anajua kuwa mimi ni mtu wa kusema ukweli. Niliposema kuhusu soko la Wakulima niliitwa majina mengi, ikiwemo kuwa mkabila. Katika soko hilo kuna wafanyabiashara kutoka jamii zote. Ninapoweka wazi matatizo haya, watu wengi wanakuwa na tatizo nami,” ameongeza.

Kuhusu uhusiano wake na Rais William Ruto, Gachagua alieleza kuwa wapinzani wake waliokuwa wakipanga mikutano ya kumwondoa madarakani mara nyingi wanadai kuwa wanaidhinishwa na Rais Ruto ili kutekeleza majukumu hayo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa hawezi kumshutumu Rais kwa kuwa hakuwa akihudhuria mikutano hiyo.

“Sijui kama anajua, lakini wengi wanataja jina lake wakisema yeye ndiye aliyetuma ujumbe wa kuidhinisha mikutano hiyo, lakini kwa kuwa hakuwepo kwenye mikutano hiyo, siwezi kumshutumu,” alisema.

Gachagua alidai kuwa chini ya utawala wa sasa, hakuna hoja yoyote ya kumwondoa madarakani ambayo inaweza kupelekwa Bungeni bila idhini ya Rais.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!