Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Iganjo mkoani Mbeya, ambacho ni sehemu ya Mradi wa Tanzania–Zambia Transmission Interconnector (TAZA), unaolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia.
Mhe. Ndejembi ameeleza hayo leo, Oktoba 16, 2026, alipotembelea kituo hicho ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme nchini.

Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa, hatua itakayochochea shughuli za uchimbaji madini, ukuaji wa viwanda, uwekezaji na kuongeza fursa za ajira, hususan kwa vijana, pamoja na kuwezesha usafirishaji wa umeme kwenda nchi jirani ikiwemo Zambia.
“Umeme utakaofika hapa si kwa ajili ya nchi jirani ya Zambia pekee, bali pia utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa. Naipongeza sana Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kazi nzuri iliyofanyika. Nilipofika hapa mwezi Machi, mradi ulikuwa katika hatua za awali, lakini kwa sasa uko mbioni kukamilika. Kwa maendeleo haya, nimeridhika na nilichokiona,” amesema Mhe. Ndejembi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya nishati ili kuimarisha upatikanaji wa umeme na kufungua fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ameeleza kuwa Kituo cha Iganjo kitakuwa na uwezo wa kusafirisha umeme kwenda maeneo yenye mahitaji makubwa ya nishati, ikiwemo Saza mkoani Songwe, ambako shughuli za uchimbaji madini zinahitaji umeme wa uhakika, pamoja na kuwezesha usafirishaji wa umeme kwenda nchi jirani ya Malawi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema ujenzi wa Kituo cha Iganjo unaogharimu takribani shilingi bilioni 175 umefikia asilimia 93, huku kituo hicho kikitarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na maeneo jirani.
“Mradi huu una umuhimu mkubwa katika kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Uyole, Mbarali, Tukuyu na Busokelo, kupitia ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme,” amesema Bw. Twange.
