Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kushiriki maziko ya Mwanafunzi wa Chuo cha utalii Marangu fani ya umeme, Mkoani Kilimanjaro, Clara Kimathi (21) aliyefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake na ‘house boy’ wa familia aliyokuwa akiishi kwa madai ya kukataa kushirikiana naye kimapenzi.
Akiongoza ibada hiyo ya maziko Machi 6,2025 iliyofanyika nyumbani kwa Marehemu Kata ya Makuyuni Mtaa wa Msufini katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Himo,Padri David Mwahiri ameitaka Jamii kuwa na Imani pamoja na kutunza haki za wengine ili kuepuka matukio ya kupora haki ya mwingine.
“Amani na haki vinaendana na hatutaki haki ya mtu ipotee,Marehemu alipambania utu wake ila yakatokea haya yaliyotokea niombe familia na Jamii izidi kuombea familia hii hasa wadogo zake waliobakia” Padri Mwahiri
Mwanafunzi huyo ambaye ni yatima alikuwa akiishi na moja ya familia iliyopo kitongoji cha Mieresini, kata ya Makuyuni Wilaya ya Moshi baada ya baba na mama yake kufariki miaka michache iliyopita.
Hata hivyo, baada ya Mwanafunzi huyo kujeruhiwa Desemba 5 mwaka jana, alikuwa amelazwa hospitali ya KCMC kwa zaidi ya miezi miwili ambapo hali yake haikutengamaa kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata mwili mwake, ambapo inadaiwa alichomwa visu vitano vya tumboni, mgongoni na kupelekea utumbo kutoka nje na ilipofika Februari 25,2025 alifariki dunia.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba lilitokea Desemba 5, mwaka jana na tayari hatua kadhaa za kisheria zilishachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.
“Desemba 5, 2024 majira ya saa tano na nusu huko maeneo ya Mieresini kata ya Makuyuni, Himo binti aitwaye Clara Kimati(21) Mwanachuo cha utalii Marangu alijeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali upande wa kushoto na tumboni na kijana wa kazi za ndani,”amesema Kamanda Maigwa
Kamanda Maigwa amedai kuwa, chanzo cha tukio hilo ni baada ya marehemu kumkatalia penzi ‘house boy’huyo.
“Kiini cha tukio hili ni kumtaka kimapenzi marehemu kwa nguvu, mbinu iliyotumika ni kumjeruhi marehemu kwa kumkata na kitu chenye nchi kali upande wa kushoto na tumboni na mtuhumiwa aitwaye Ezekiel Komba baada ya kutenda kosa hilo na alitaka kujiua kwa kukata koromeo,”amesema Maigwa