Latest Posts

NSSF YAANIKA MIKAKATI YA KUIFIKIA SEKTA ISIYO RASMI KUJIUNGA NA HIFADHI YA JAMII KAMA NJIA YA KUONDOKANA NA UMASIKINI NCHINI

Wawakilishi wa vyombo mbalimbali vya habari wakipokea cheti kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) cha kuwatambua kama wawasilishaji wazuri wa michango ya wanachama leo Jumatatu Oktoba Mosi, 2024 kwenye mkutano baina ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Bw. Masha Mshomba na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari katika ukumbi wa NSSF Mafao House Ilala jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba akiongea na wahariri wa vyombo vya habari (hawapo pichani) katika kikao kazi leo Jumanne Oktoba Mosi, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa NSSF Mafao House

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia kaa makini hotuba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba (hayupo pichani) leo Jumanne Oktoba Mosi, 2024 katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa NSSF Mafao House

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile akiongea wakati wa kikao kazi baina ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba na wahariri wa vyombo vya habari leo Jumanne Oktoba Mosi, 2024 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa NSSF Mafao House
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Lulu Mengele akitoa neno la ukaribisho kwa wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari kwenye kikao kazi na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Bw. Masha Mshomba leo Jumanne Oktoba Mosi, 2024 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa NSSF Mafao House

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeweka wazi mikakati yake itakayopelekea nchi ya Tanzania inafikia kwa kiwango kikubwa sekta isiyo rasmi katika suala la hifadhi ya jamii lengo likiwa ni kuondoa umasikini.

 

Hayo yamesemwa leo Jumanne Oktoba Mosi, 2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Bw. Masha Mshomba, katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari ambapo amesisitiza kuwa, hifadhi ya jamii ni moja ya nguzo kuu ya kuondoa umasikini.

 

Ameongeza kwa kusema kuwa, katika kufikia lengo la kuifikia sekta isiyo rasmi kwa kikubwa wao kama Mfuko wameamua kubadilisha utaratibu kwa lengo la kurahisisha utaratibu wa kujiunga na kuwafikia kupitia wizara, taasisi na vyama mbalimbali vya kijamii.

 

Sambamba na hayo Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF ameeleza kuwa,

pamoja na wajibu huo lakini pia wanaendelea na majukumu yao ya msingi ya hifadhi ya jamii ikiwemo kukusanya michango kutoka kwa waajiri kuandikisha wanachama na waajiri na kisha kuwekeza michango hiyo ili kuuwezesha kutimiza jukumu la msingi la kutoa mafao.

 

 

Vilevile ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa uliochangia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha takribani miaka minne.

 

Mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la thamani ya Mfuko kutoka shilingi 4.8 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 8.5 hivi sasa sawa na ukuaji wa zaidi ya asilimia 70.

 

Katika kutekeleza maelekezo ya Serikali ya taasisi za umma kutumia mifumo kwenye utendaji kazi wake wa kila siku, Bw. Mshomba amesema

 

“Tumekuwa tukijitahdi kuweka mifumo ya TEHAMA kwenye huduma zetu zote, na niwaambie tu kwamba mwishoni mwa mwaka 2024/2025 tunatarajia shughuli na huduma zetu zote zitatolewa kupitia mifumo ya TEHAMA” alisema na kuongeza

 

“Kwa sasa huduma na shughuli zetu zinafanyika kupitia mifumo kwa kiwango cha asilimia 82, ni kiwango kikubwa cha matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma na kufanya shughuli zetu kutoka asilimia takribani 42.”

 

Ameendelea kwa kufafanua kuwa, Kupitia TEHAMA wameweza kuwafikia wateja wengi na kwa sasa wateja hao hawalazimiki kufika kwenye ofisi za NSSF kwani hivi sasa, wanachama na waajiri wanaweza kujihudumia kupitia mifumo ikiwemo kuwasilisha michango ya wanachama na mwanachama anaweza kuangalia idadi ya michango iliyowasilishwa.

 

Katika kurahisisha na kuboresha huduma kwa wateja, Bw. Mshomba ametanabaisha kuwa, hivi karibuni NSFF imetambulisha huduma mpya ya kuomba na kufuatilia mafao kwa njia ya mtandao pasi na kufika katika ofisi zao lengo likiwa ni kuwaondolea usumbufu wanachama wake hususan wastaafu ambao wengi wao wana umri mkubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Omar Mziya amesema madhumuni ya kuanzishwa kwa Skimu ya Sekta Binafsi ni pamoja na

uongeza wigo wa Hifadhi ya Jamii kwa makundi ambayo hayanufaiki na huduma zao ingawa wanashiriki kikamilifu kuchangia uchumi wa nchi, kusaidia juhudi za serikali za kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi.

 

Madhumuni mengine ni kuongeza nguvu za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa nchi na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

 

Bw. Mziya ametaja Vigezo vya kujiunga na Skimu hiyo kuwa Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 15 hadi 70 na asiwe ni mnufaika wa mafao ya pensheni kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini lakini pia ni lazima aw awe na namba ya NIDA au kitambulisho chochote kinachomtambua (leseni ya udereva/mpiga kura na kuwa na picha ndogo moja (Passport size).

 

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameipongeza NSSF kwa kazi nzuri na uwekezaji wanaofanya ambao una tija kwa jamii na Taifa.

 

Ametolea mfano uwekezaji wa daraja la Nyerere ambapo amesema hivi sasa hakuna magonjwa anayepoteza maisha kwa kusubiria kuvuka kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na badala yake wananchi wenye kadhia hiyo hutumia daraja na kuwafikisha wagonjwa hospitali haraka.

 

Aidha, Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la Wahariri ameipongeza NSSF kwa kufanya maboresho makubwa katika utendaji kazi ikiwemo kwenye matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma.

 

Kando na hayo, ametoa wito kwa Wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati jambo ambalo anaamini kuwa, linawezekana.

 

Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo Rasmi (National Informal Sector Scheme-NISS) imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Sura ya 50 marejeo ya mwaka 2018 kwa madhumuni ya kuhudumia wananchi waliojiajiri wenyewe katika shughuli za kiuchumi.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!