Latest Posts

NYANGWINE APATA TENA CHETI, AFANIKISHA ZAIDI YA MILIONI 27 KUPATIKANA KATIKA HARAMBEE YA KANISA LA MENNONITE

Madiwani wamwagia sifa, mmoja asema ameleta mvua

Aeleza waliomsaidia kupatanisha koo mwaka 2010, asisitiza amani, umoja na mshikamano

Na Helena Magabe, Tarime

Mdau wa maendeleo na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nyambari Nyangwine, amepewa tena cheti na Kanisa la Mennonite lililopo katika Kijiji cha Mangucha, Kata ya Nyanungu, wilayani Tarime, baada ya kuwa mgeni rasmi wa harambee iliyofanikisha kupatikana kwa shilingi 27,290,150 pamoja na mifuko 15 ya saruji.

Nyangwine amechangia shilingi milioni 10, huku akiungwa mkono na madiwani waliotoa shilingi 1,000,000, Mwenyekiti wa Halmashauri, Simion Kilesi, aliyetoa shilingi 500,000, Diwani wa Kata hiyo, Tiboche Richard, aliyetoa shilingi 500,000, pamoja na Christopher Kangoye, aliyetoa shilingi 300,000. Padre wa Nyamwaga na Masista wawili wamechangia shilingi 300,000, huku waumini wakichangia zaidi ya shilingi 2,000,000. Pasco Maswi ametoa mifuko 5 ya saruji, na wachangiaji wengine wameongeza mifuko 10.

Kwa upande mwingine, Nyangwine ameahidi kuchangia shilingi milioni 12 kwa makanisa manne, ambapo kila kanisa kitapata shilingi milioni 3. Makanisa yaliyonufaika ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanisa la Anglikana, Kanisa Katoliki (RC), na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA). Ameeleza kuwa ametoa mchango huo kwa hiari yake bila kuombwa.

Diwani wa Kata ya Bumera, Deogratius Ndege, amesema kuwa Nyangwine anajishughulisha na masuala ya kiroho, ikiwa ni pamoja na kugawa vitabu bure mashuleni na kusaidia makanisa. Amesema kuwa mara mbili alipoandaa harambee, mvua imenyesha, jambo ambalo waumini wameliona kama baraka.

Diwani wa Kata ya Nyamwaga, Mwita Magige, amesema kuwa Nyangwine amewahi kufanya harambee mara mbili katika Kanisa la Roman Catholic Nyamwaga, ambako pia anapendwa sana.

Diwani wa Viti Maalumu kutoka Tarafa ya Ingwe, Mariamu Mkono, amesema kuwa kitendo cha Nyangwine kutunukiwa tena cheti ni ishara ya moyo wake wa kujitolea kusaidia jamii. Madiwani wote wamempongeza kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya dini na elimu.

Katika hotuba yake, Nyangwine amemshukuru Askofu Amos Joseph Muhagaji wa Dayosisi ya Shirati, mzaliwa wa Nyanungu, ambaye amehudhuria harambee hiyo. Ametaja pia Mzee Christopher Kangoye kuwa ni miongoni mwa waliomsaidia kumaliza mgogoro wa koo mwaka 2010 alipokuwa Mbunge wa Tarime kabla ya jimbo hilo kugawanywa mara mbili.

Ameomba viongozi wa dini kukemea wale wanaoweza kuchochea migogoro ya koo wilayani Tarime, akisisitiza umuhimu wa amani, mshikamano na maendeleo.

Askofu wa Kanisa la Mennonite, Dayosisi ya Tarime, Albert Jera Randa, amemkabidhi Nyangwine cheti hicho Machi 9, 2025. Hii ni siku moja tu baada ya kutunukiwa cheti kingine Machi 8, 2025, kutoka kwa kikundi cha waigizaji wa filamu ya Himaya ya Nyakonga.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!