Latest Posts

NYANGWINE ASISITIZA MAADILI KWA JAMII, ATUMIA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 18 KUCHANGIA MAKANISA

– Atunukiwa cheti na waigizaji wa filamu ya Himaya ya Nyakonga

Na Helena Magabe, Tarime

Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nyambari Nyangwine, Machi 8, 2025, alitoa mchango wa zaidi ya shilingi milioni 18 kwa makanisa mbalimbali wilayani Tarime, mkoani Mara.

Makanisa aliyoyachangia ni EAGT Sirari Bondeni lililopo kata ya Sirari, pamoja na makanisa mawili ya Waadventista Wasabato, ambayo ni Kanisa la Nyabitocho, kata ya Mbongi, na Kanisa la Koryuba Mlimani, mtaa wa Nyabitocho, kata ya Pemba.

Katika Kanisa la EAGT Sirari Bondeni, Nyangwine aliombwa kuchangia shilingi 1,600,000 kwa ajili ya vifaa vya kwaya, lakini alitoa shilingi milioni 2. Aidha, katika harambee ya ujenzi wa kibweta cha makambi katika Kanisa la Nyabitocho, kata ya Mbongi, ambapo alikuwa mgeni rasmi, alichangia shilingi milioni 10. Pia, alitoa shilingi milioni 2 kwa Kanisa la Koryuba Mlimani.

Harambee hiyo ilihudhuriwa na madiwani waliotoa jumla ya shilingi 900,000, huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime Vijijini, Simion Kilesi, akichangia shilingi 500,000. Akizungumza katika harambee hiyo, Kilesi alisema, “Kutoa ni kubarikiwa.”

Mchango mwingine ulikuwa kutoka kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Mugini Jacob, aliyetoa shilingi 100,000, huku Jackson Kangoye akitoa shilingi 100,000 na Christopher Kangoye shilingi 200,000. Michango mingine kutoka kwa wadau mbalimbali ilifanya jumla ya fedha zilizopatikana katika Kanisa la Nyabitocho kufikia shilingi milioni 13.5.

Mchungaji wa EAGT Sirari Bondeni, Boniphace Mkirya, alimshukuru Nyangwine kwa mchango wake na kumpatia maji ya kunywa kabla ya safari yake kuelekea Nyabitocho. Naye Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Nyabitocho, Kumba Kihiri, alimshukuru kwa msaada wake na kumuombea baraka kwa tendo lake la kuchangia ujenzi wa kibweta, ambalo linatarajiwa kutumika mwaka huu katika makambi.

Katika hotuba yake, Nyangwine aliwaasa wananchi kudumisha maadili mema na kuepuka kutumia mitandao ya kijamii kwa lugha za matusi dhidi ya wanasiasa. Pia, aliwataka vijana kusoma kwa bidii na kujiandaa kujiajiri. Aidha, aliwataka wakazi wa Tarime kulinda amani na kuachana na siasa za mgawanyiko kwa misingi ya koo.

Baada ya harambee hiyo, Nyangwine alitembelea kata ya Nyakonga, ambako alikamilisha ahadi yake ya kuchangia filamu ya Himaya ya Nyakonga. Awali, alikuwa ameahidi shilingi milioni 5, na Machi 8 alikamilisha ahadi hiyo kwa kutoa shilingi milioni 1 iliyobaki.

Uzinduzi wa filamu hiyo ulifanyika hivi karibuni, ambapo Nyangwine aliombwa kuwa mgeni rasmi, lakini alituma mwakilishi wake, Daniel Magita, kuhudhuria kwa niaba yake.

Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simion Kilesi, alimshukuru Nyangwine kwa mchango wake, akisema maendeleo hayatokoma Nyakonga. Naye Mwenyekiti wa kikundi cha filamu hiyo, Chacha Ryoba Isaya, alimkabidhi Nyangwine cheti cha shukrani, akisema mchango wake wa shilingi milioni 4 uliwawezesha kuzindua filamu hiyo na kununua vifaa vya kazi kama kompyuta na kamera.

Katika hatua nyingine, Nyangwine aliwaahidi wasanii hao safari ya mafunzo jijini Dar es Salaam ili kujifunza kutoka kwa wasanii wakongwe. Kikundi hicho kina jumla ya wasanii 30, wakiwemo wanawake 7 na wanaume 23.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!