Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, ameungana na mamia ya viongozi na watu wenye ushawishi duniani kutoa pongezi kwa Donald Trump kwa kushinda kiti cha Urais nchini Marekani.
Kupitia taarifa maalum, Obama na mkewe, Michelle Obama, wamempongeza Trump pamoja na Seneta JD Vance kwa ushindi wao katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.
Obama amesisitiza kuwa, licha ya tofauti za kisiasa zilizopo kati ya chama chake cha Democratic na chama cha Republican cha Trump, misingi ya demokrasia inawataka wote kukubali matokeo kwa amani. Obama ameeleza kuwa kukubali matokeo ni sehemu ya demokrasia na kuheshimu ushindi wa mpinzani ni ishara ya mshikamano wa taifa.
Aidha, Obama ameongeza kuwa sasa ni wakati wa kuzingatia misingi ya kikatiba, kusikiliza maoni ya kila mmoja, na kuvumiliana kama taifa.
“Katika nchi kubwa na tofauti kama yetu, hatutakubaliana kila mara kwa kila jambo. Lakini maendeleo yanahitaji sisi kuwa na nia njema na uvumilivu hata kwa wale tunaotofautiana nao sana. Hivyo ndivyo tumefika mbali hivi, na hivyo ndivyo tutaendelea kujenga nchi ambayo ni ya haki zaidi, usawa zaidi na uhuru zaidi”, amesema.