Latest Posts

ODINGA ATUMWA SUDAN KUSINI BAADA YA MAKAMU WA RAIS WA NCHI HIYO KUKAMATWA

Habari za kukamatwa kwa Riek Machar, Makamu wa Rais wa nchi ya Sudan Kusini ambaye ni kiongozi wa Sudan People’s Liberation Movement in Opposition (SPLM-IO), zilizua taharuki kimataifa huku mashirika na mataifa yakiharakisha juhudi za kuzuia mgogoro huo kuzorota zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa, hali ya wasiwasi ilikuwa imeanza kujitokeza kwa miezi kadhaa kabla ya tukio hilo, huku vikosi vya usalama vinavyomuunga mkono Rais Salva Kiir vikiripotiwa kuizingira nyumba ya Machar.

Jumatano usiku, taarifa kutoka kwa Msemaji wa Machar, Puok Both Baluang, na Naibu Kiongozi wa SPLM-IO, Oyet Nathaniel Pierino, zilieleza kuwa msafara wa magari 20 yenye silaha nzito uliingia nyumbani kwa Machar ukiongozwa na waziri wa ulinzi na mkuu wa usalama wa taifa.

Baada ya hapo, walinzi wa Machar walinyang’anywa silaha, na hati ya kukamatwa kwake ikatolewa chini ya mashtaka ambayo hayakuwa wazi.

Huku wasaidizi wake wakikamatwa na kupelekwa kusikojulikana, Machar na mkewe waliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani, hali ambayo chama chake kimeeleza kuwa ni uvunjaji wa Mkataba wa Amani wa 2018.

Kulingana na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini (UNMISS), tukio hili linaweza kuipeleka nchi hiyo kwenye vita vipya.

Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD), iliyofanikisha mkataba wa amani wa 2018, ilitoa tahadhari ikisema kuwa hali ikiendelea hivi, mchakato wa mpito unaweza kuvunjika na nchi ikaingia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Serikali ya Marekani, kupitia Bureau of African Affairs, ilitoa wito kwa Rais Kiir kufuta hatua hiyo mara moja.

Kenya, ambayo imekuwa mstari wa mbele katika mazungumzo ya amani Sudan Kusini, imechukua hatua ya haraka kwa kumtuma Raila Odinga kama mjumbe maalum. Kupitia ujumbe wa mtandao wa kijamii, Rais William Ruto amesema:

“Nilizungumza kwa simu na Rais Salva Kiir kuhusu hali ya Sudan Kusini na kukamatwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar. Baada ya mashauriano na Rais Museveni na Waziri Mkuu Abiy Ahmed, ninamtuma mjumbe maalum Sudan Kusini kwa mazungumzo na kutupatia taarifa ya hali ilivyo.”

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, ametangaza kuwa atajumuisha Jopo la Hekima la AU, linaloongozwa na Jaji Mstaafu wa Kenya, Effie Owuor, katika juhudi za kutatua mgogoro huo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!