Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda, amewataka wananchi kuendeleza ushirikiano, kubadilishana uzoefu na mawazo yatakayowezesha mabadiliko chanya katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Akizungumza Agosti 2, 2025, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mkoani Morogoro, Pinda amesisitiza kuwa maendeleo endelevu katika sekta hizo yanahitaji mshikamano kati ya sekta binafsi na ya umma, hasa kwenye maeneo ya uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao.

“Sekta binafsi na ya umma zinapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuinua tija katika kilimo, mifugo na uvuvi. Ushirikiano huu utasaidia kuongeza thamani ya mazao na kuboresha maisha ya wananchi”, ameeleza Pinda.
Ameongeza kuwa ili Watanzania wanufaike ipasavyo na maendeleo ya kisekta, ni lazima watumie teknolojia za kisasa na kuachana na matumizi ya jembe la mkono. Aidha, amehimiza uwekezaji wa sekta binafsi kwa kuwapatia maeneo mahsusi ya kuwekeza.

Akitaja mafanikio yaliyopatikana kupitia sekta ya kilimo, Pinda amesema baadhi ya mazao yaliyoongeza mapato ya serikali ni pamoja na tumbaku iliyochangia takribani trilioni 2.2, korosho- bilioni 931 pamoja na mazao mengine kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Katika hatua nyingine, Pinda amewahimiza Watanzania wote kujitokeza kushiriki uchaguzi mkuu ujao mwezi Oktoba 2025, akisisitiza kuwa ni haki yao ya msingi ya kikatiba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amemshukuru Pinda kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kushiriki ufunguzi wa maadhimisho hayo huku akiahidi kuwa mkoa utaendelea kujipanga kuhakikisha mafanikio yanapatikana kupitia sekta hizo.

Maonesho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, 2025.”