Na Theophilida Felician, Kagera.
Jeshi la Polisi mkoani Kagera limekipongeza Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania (TAMESOT) kwa juhudi zake za kuelimisha waganga wa tiba asili kuhusu weledi, maadili ya taaluma yao na mapambano dhidi ya vitendo vya kihalifu vinavyofanywa kwa kivuli cha tiba asili.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya TAMESOT kwa waganga wa tiba asili yaliyofanyika katika Manispaa ya Bukoba, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Adriano Modestusi, kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, amesema elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa inalenga kuwajengea waganga uelewa wa sheria, heshima na uwajibikaji kwa jamii.

Aidha, aliwakumbusha waganga kuwa kufanya kazi bila kuwa na leseni halali ni kosa la kisheria na Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua wote wanaokiuka taratibu hizo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TAMESOT Taifa, Bw. Lukas Joseph Mlipu, ambaye pia ni mkufunzi wa mafunzo hayo, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano waliouonyesha katika kutoa elimu hiyo kwa vitendo, akisema hatua hiyo imeimarisha kazi ya chama katika maeneo mbalimbali nchini.
Bw. Mlipu amesema mafunzo hayo yalihusisha masomo mawili kutoka katika vitabu maalum, mojawapo likiwa la miongozo kwa viongozi wa tiba asili, na la pili likiwa kwa waganga wote kwa ujumla, likilenga kuongeza uelewa kuhusu taratibu, sheria na maadili ya kazi zao.

Ametoa wito kwa waganga wote kushirikiana na vyombo vya dola kwa kuwabaini watu wanaojiita waganga lakini wanajihusisha na vitendo vya kihalifu na utapeli, hatua ambayo itasaidia kulinda heshima ya tiba asili nchini.
Viongozi wa waganga kutoka maeneo mbalimbali akiwemo Adamu Kataga (Muleba), John Shigera (Misenyi), Meli Agustino (Bukoba Mjini) na Ramadhani Rashidi, Katibu wa TAMESOT Wilaya ya Misenyi, wameshukuru kupata mafunzo hayo wakisema yamewaongezea maarifa na uelewa wa kitaaluma, na wameahidi kutoa ushirikiano kwa serikali na chama.

Katika hatua nyingine, Bw. Mlipu ametumia nafasi hiyo kuhamasisha waganga kujitokeza kwa wingi kushiriki Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika itakayofanyika Dodoma kuanzia Agosti 25 hadi 31, 2025, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.