Kuelekea sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema limejipanga ipasavyo katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa kufanya misako na doria za magari, pikipiki, mbwa wa Polisi na miguu katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ili kuzuia na kudhibiti uhalifu na wahalifu.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Benjamin Kuzaga wakati akizungumzia maandalizi kuelekea sikukuu ya sikukuu ya Pasaka.
Kamanda Kuzaga amesema katika nyumba za ibada hususani kanisani, Jeshi la Polisi limejipanga kwa kushirikiana na kamati za usalama katika maeneo hayo, katika makazi ya wananchi na kwamba Polisi inaendelea na utaratibu wa kufanya doria kwa kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyopo katika maeneo hayo ambapo katika kumbi za starehe polisi imewahimiza wamiliki kuweka walinzi binafsi pamoja na kuzingatia taratibu zote za uendeshaji wa biashara zao kwa mujibu wa leseni na vibali ili kuhakikisha kunakuwa na usalama.
Aidha, kwa upande wa usalama barabarani, kamanda wa Polisi Mbeya amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia usalama wao kwanza na utii wa sheria za usalama barabarani bila shuruti ili kuepuka ajali na kwamba ni marufuku kwa Dereva kutumia kilevi, Jeshi la Polisi limejipanga kutumia vipima ulevi kukabiliana na madereva watakaotumia vileo na kuendesha vyombo vya moto, pia Jeshi la Polisi limejipanga kudhibiti makosa hatari kama vile mwendo kasi na “wrong overtaking” hasa katika maeneo hatarishi kama vile mlima nyoka, mlima Iwambi, Igawilo na barabara ya Mbeya – Chunya.
Ameonya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya yeyote atakayekamatwa kwa kukiuka sheria za usalama barabarani na kutoa rai kwa wazazi na walezi katika msimu huu wa sikukuu kuzingatia ulinzi na usalama wa mtoto kwa kuhakikisha wanaimarisha uangalizi wa watoto ili kuwaepusha na mazingira hatarishi.
“Hatutegemei kuona watoto wanazurura hovyo mitaani bila kuwa na uangalizi, kwenye sehemu za michezo ya watoto tunatarajia kuwaona wazazi/walezi wakiwa na watoto wao ili kuangalia usalama wao. Sambamba na hayo, katika maeneo yenye fukwe kama vile Matema, Ngonga – Wilaya ya Kyela, Kisiba – Wilaya ya Rungwe na Ziwa Ngosi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya litaimarisha ulinzi pia linawataka wamiliki wa maeneo hayo kuweka walinzi na waangalizi kwani katika kipindi hiki kunatarajiwa kuwa na idadi kubwa ya watu wa rika tofauti watakaofika maeneo hayo kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Pasaka”, ameeleza kamanda Kuzaga.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawataka wananchi kuzingatia usalama wao kwani ulinzi unaanza na mtu mmoja mmoja na kwamba kwa upande wa Polisi wamejipanga imara na linawahakikishia usalama wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya, wageni watakaofika kwenye mkoani Mbeya na hata wale watakaopita kuelekea mikoa jirani na nchi jirani kwa kutumia barabara ya TANZAM inayounganisha nchi ya Tanzania, Malawi, Zambia hadi Afrika ya Kusini.