Watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Al-Shabab, kundi lenye mafungamano na Al-Qaeda, wamevamia kambi ya polisi katika Kaunti ya Garissa, mashariki mwa Kenya, na kuwaua polisi sita huku wengine wanne wakijeruhiwa, mamlaka imethibitisha.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi iliyotumwa kwa vyombo vya habari, shambulio hilo lilitokea Jumapili alfajiri, ambapo washambuliaji waliwashambulia askari waliokuwa kambini kwa kutumia silaha mbalimbali na kufanikiwa kuiteka kambi hiyo kwa muda.
“Watu sita wamefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa na wako hospitalini,” ripoti ya polisi imeeleza.
Kundi la Al-Shabab mara kwa mara limekuwa likitekeleza mashambulizi katika maeneo ya mpakani kati ya Kenya na Somalia, likilenga jeshi, polisi na raia wa kawaida.
Katika hatua nyingine, Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umetangaza tahadhari kwa raia wake Jumanne, ukiwataka kuepuka kusafiri katika maeneo yenye hatari ya ugaidi, yakiwemo Garissa na kaunti nyingine zinazopakana na Somalia.
Kwa miaka kadhaa, Al-Shabab imekuwa ikipambana na serikali ya Somalia kwa lengo la kuipindua na kuanzisha utawala wake katika eneo la Pembe ya Afrika.
Wakati huohuo, watu wasiopungua 44 wameuawa na wengine 13 kujeruhiwa vibaya baada ya wanamgambo kuvamia msikiti nchini Niger, mamlaka ya ulinzi imesema.
Shambulio hilo lilitokea siku ya Ijumaa wakati wa sala za alasiri katika kijiji cha Fombita, kilicho katika eneo la Kokorou, karibu na mpaka wa Niger, Burkina Faso na Mali.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Niger, washambuliaji walizingira msikiti huo na kuwaua waumini kwa ukatili wa hali ya juu, kabla ya kuchoma soko na nyumba za wananchi. Mamlaka ililaumu kundi la EIGS, tawi la Daesh lililo na mizizi katika eneo hilo, kwa kuhusika na shambulio hilo.
Uasi wa wanamgambo katika eneo la Sahel ulianza mwaka 2012 baada ya waasi wa Tuareg kuchukua udhibiti wa kaskazini mwa Mali. Tangu wakati huo, ghasia zimeenea hadi nchi jirani kama Burkina Faso na Niger, pamoja na baadhi ya mataifa ya pwani ya Afrika Magharibi kama Togo na Ghana.
Machafuko haya yamesababisha vifo vya mamia ya maelfu ya watu na mamilioni kuyahama makazi yao.
Kwa kushindwa kudhibiti usalama, serikali za Mali, Burkina Faso na Niger zimekumbwa na mapinduzi ya kijeshi kati ya 2020 na 2023. Mataifa haya yote matatu kwa sasa yanaongozwa na serikali za kijeshi, licha ya shinikizo la kimataifa la kutaka warejee kwenye utawala wa kiraia.
Tangu mapinduzi hayo, nchi hizo zimejitenga na mataifa ya Magharibi na badala yake zimeelekeza macho kwa Urusi kwa msaada wa kijeshi.