Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeyanowa makundi mbalimbali mkoani Mtwara, ikiwemo makundi maalumu ya watu wenye ulemavu na wajasiriamali, kuhusu namna ya kuchangamkia fursa za zabuni zinazotangazwa na Serikali kupitia idara za ununuzi.
Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bahati Geuzye, amesema mafunzo ya aina hiyo ni nadra kufanyika, hivyo ni muhimu kwa wadau wanaopata nafasi kuyahudhuria ili kuongeza uelewa na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wadau hao muhimu kutambua fursa zilizopo katika sekta ya ununuzi wa umma, hususan wanawake, vijana, wazee, watu wenye ulemavu, wazabuni pamoja na watumishi wa ngazi za msingi ambapo Mafunzo hayo yamefanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Geuzye ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Serikali hutumika katika manunuzi ya umma, hivyo Serikali imechukua hatua madhubuti kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa na nia njema anapata haki na fursa ya kushiriki na kunufaika kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Tunashukuru sana PPRA kwa kutupa kipaumbele na kuendesha mafunzo haya yenye lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi na kutoa fursa sawa kwa wote.”Amesema Geuzye.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka PPRA Magnus Steven, alisema mafunzo hayo yalianza Novemba 10, 2025, katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, na yanaendelea kutolewa katika halmashauri zote tisa za mkoa huo.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwapatia elimu washiriki kuhusu sheria na kanuni za ununuzi wa umma, namna ya kuomba zabuni, na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa Serikali (NeST), ili kuongeza uwazi na ufanisi katika michakato ya manunuzi.
Ameeleza kuwa mamlaka hiyo imezielekeza taasisi zote nunuzi nchini kutenga asilimia 30 ya fursa za zabuni kwa makundi maalumu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha kiuchumi na kuwajengea uwezo wa kushindana katika soko la manunuzi ya umma.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru PPRA na Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo,Fatuma Mpondomoka mmoja wa washiriki, amesema elimu hiyo imewapa mwanga wa namna ya kuchangamkia fursa mbalimbali za zabuni zinazotangazwa na Serikali.
“Tumejifunza mengi kupitia mafunzo haya; sasa tunafahamu hatua za kuchukua ili kushiriki kwenye zabuni kwa uhalali,” alisema Fatuma.
Naye Mustafa Yasini alisema mfumo wa NeST utawasaidia kufahamu kwa urahisi kuhusu fursa za manunuzi na namna bora ya kuomba zabuni serikalini.
“Kwa sasa tutakuwa na uelewa mpana kuhusu mfumo wa ununuzi wa Serikali ni fursa kwetu kujua namna bora ya kushiriki kwenye tenda mbalimbali.”Amesema Mustafa.