Prince Rahim Al-Hussaini, anayejulikana pia kama Prince Rahim Aga Khan, ametangazwa rasmi kuwa Imam wa 50 wa Waismailia wa Kishia, kutokana na kufunguliwa kwa wosia wa baba yake, Prince Karim Aga Khan IV, siku ya Jumatano. Taarifa hiyo imetolewa na Aga Khan Development Network (AKDN).
Tangazo hili limekuja baada ya kifo cha Prince Karim Aga Khan IV, aliyefariki Jumanne jijini Lisbon, Ureno, akiwa na umri wa miaka 88. Lisbon ni makao makuu ya Imamat ya Waismailia.
Prince Rahim Aga Khan, aliyekuwa mzaliwa wa Oktoba 12, 1971, ndiye mtoto wa kwanza wa marehemu Aga Khan IV na mke wake wa kwanza, Princess Salimah, aliyewahi kuwa mwanamitindo wa Uingereza kwa jina la kuzaliwa Sarah Croker Poole. Wanandoa hao walizaa watoto watatu- binti mmoja na wana wawili.
Kwa muda mrefu, Prince Rahim Aga Khan amekuwa sehemu muhimu ya taasisi mbalimbali ndani ya mtandao wa Aga Khan Development Network (AKDN). Amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, akihudumu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira na Tabianchi ya AKDN.
Jamii ya Waismailia duniani inakadiriwa kuwa na zaidi ya wafuasi milioni 15, wanaoishi katika maeneo mbalimbali kama Asia ya Kati, Mashariki ya Kati, Kusini mwa Asia, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Ulaya, na Amerika Kaskazini.
Kabla ya tangazo la uongozi mpya, AKDN ilitangaza kifo cha Prince Karim Aga Khan IV kupitia mtandao wa X (zamani Twitter).
Aga Khan IV, aliyekuwa Imam wa 49 wa Waismailia, alikuwa maarufu si tu kwa uongozi wake wa kiroho bali pia kwa utajiri wake mkubwa na mchango wake katika maendeleo ya jamii mbalimbali duniani. Alikuwa mpenzi wa mashindano ya farasi na miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni kumiliki farasi maarufu wa mbio, Shergar.
Mbali na burudani, alikuwa pia mfadhili wa miradi mingi ya maendeleo duniani, akitumia mamilioni ya dola kusaidia jamii maskini zaidi.
Prince Karim Aga Khan IV alizaliwa Desemba 13, 1936, jijini Geneva, Uswisi, lakini alitumia sehemu kubwa ya utoto wake Nairobi, Kenya.
Baadaye alirejea Uswisi na kusoma katika shule ya kifahari ya Le Rosey, kisha akaenda Harvard University nchini Marekani kusomea historia ya Uislamu.
Aliingia katika uongozi wa kidini akiwa na umri wa miaka 20 mwaka 1957, baada ya kufariki kwa babu yake, Sir Sultan Mahomed Shah Aga Khan. Babu yake alimchagua yeye kuwa Imam wa Waismailia badala ya baba yake, Prince Aly Khan, ambaye alijulikana kwa maisha yake ya kifahari na ndoa yake na muigizaji maarufu wa Hollywood, Rita Hayworth.