Latest Posts

RAIS MUSEVENI AKUTANA NA WAWAKILISHI WA STARLINK, AWAALIKA KUWEKEZA UGANDA

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amesema Jumanne kuwa amefanya kikao “chenye mafanikio” na wawakilishi wa kampuni ya intaneti ya satelaiti ya Elon Musk, Starlink, ambayo inapanua huduma zake barani Afrika na sasa inalenga kuanzisha uwepo rasmi nchini Uganda.

Kupitia ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Museveni alisema: “Ninathamini dhamira yao ya kutoa huduma ya intaneti ya gharama nafuu kwenye maeneo yasiyofikika kirahisi na kuanzisha uwepo hapa Uganda. Wamekaribishwa.”

Starlink, ambayo ni tawi la kampuni ya anga ya SpaceX, tayari inatoa huduma katika zaidi ya nchi kumi na mbili barani Afrika, na mwezi huu ilipatiwa leseni kufanya kazi nchini Somalia na Lesotho.

Uganda imekuwa ikikumbwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa watumiaji kuhusu gharama kubwa na huduma duni ya intaneti, hali ambayo inahusishwa na ushindani mdogo katika soko la mawasiliano.

Haijabainika wazi iwapo Starlink tayari imewasilisha maombi rasmi ya leseni ya kufanya kazi nchini humo. Msemaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Uganda (UCC) hakujibu maombi ya maoni kutoka kwa shirika la habari la Reuters.

Kwa sasa, kampuni tanzu ya MTN kutoka Afrika Kusini ndiyo mwekezaji mkuu katika soko la huduma za data nchini Uganda, ikishindana moja kwa moja na kampuni tanzu ya Bharti Airtel kutoka India.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!